Muziki unatibu msongo wa mawazo - utafiti

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 12:49 PM Oct 25 2024
Watafiti kutoka nchi ya Norway, Ethiopia na Tanzania wakiwa katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo( TaSUBa) kilichopo mkoani Pwani, kujadili namna Utafiti katika Muziki utasaidia kusaidia Afya ya akili na Mwili mahali pa kazi
Picha: Grace Mwakalinga
Watafiti kutoka nchi ya Norway, Ethiopia na Tanzania wakiwa katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo( TaSUBa) kilichopo mkoani Pwani, kujadili namna Utafiti katika Muziki utasaidia kusaidia Afya ya akili na Mwili mahali pa kazi

MUZIKI una faida nyingi kwa afya ya akili na kimwili, ikiwamo kupunguza msongo wa mawazo na wasiwasi, utafiti umebaini.

Imebainika kuwa kusikiliza muziki kwa utulivu hupunguza viwango vya homoni ya cortisol ambayo hushughulikia msongo wa mawazo na kuleta hali ya utulivu kimetaboliki.

Pia una uwezo wa kuboresha afya ya akili kwa kupunguza unyongevu na kuongeza hisia za furaha na motisha na hata kupunguza maumivu kimwili.

 Utafiti umebaini kuwa wagonjwa wanaosikiliza muziki wakati wa matibabu ya kimwili, hupata maumivu kidogo kuliko wale wasio na muziki. Muziki unaweza kuimarisha afya ya moyo kwa kupunguza shinikizo la damu.

 Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kushirikiana na watafiti wenza kutoka Norway, chini ya Prof. Bente Elisabeth Moen, Prof. Viggo Kruger na Prof. Brynjulf Stige, wanakusudia kufanya utafiti unaohusisha namna muziki unavyoweza kutumika mahali pa kazi kama kinga ya matatizo ya mishipa na misuli (work-related musculoskeletal disorders) na hivyo kuboresha afya ya akili na kimwili mahali pa kazi.

 Hatua hii inakuja wakati ambao kumekuwa na ongezeko la matatizo ya mishipa na misuli yakiambatana na matatizo ya afya ya akili, hasa miongoni mwa wafanyakazi.

Mtaalamu wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi wa MUHAS, Dk. Israel Nyarubeli, alikiri kuwa matatizo ya mishipa na misuli mahali pa kazi yamekuwa yanaongezeka hasa kwa nchi zinazoendelea kwa takribani asilimia 50 hadi 70 ya wafanyakazi wa sekta mbalimbali.

Alisema ripoti hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), akidokeza kuwa takribani asilimia 15 ya nguvukazi iliripotiwa kuwa na changamoto ya afya ya akili mwaka 2019 na hivyo kuhitaji mbinu madhubuti za kuzuia matatizo hayo.
 

Prof. Brynjulf Stige kutoka Kitivo cha Tiba ya Music Chuo Kikuu cha Bergen nchini Norway akizungumza na wadau wa sekta ya Afya kutoka nchi ya Tanzania na Ethiopia kwa kushirikiana na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo( TaSUBa).
Alisema tiba muziki inatumika kwa ustadi maalumu, ikiwa ni njia inayofanya kazi vizuri katika kuboresha hali ya akili, akieleza kuwa utafiti uliofanywa katika mataifa kama Norway, umeonesha ufanisi wa mbinu hiyo katika kupunguza matumizi ya dawa za maumivu na kuimarisha afya.

 "Katika mkutano wa mwaka 2023, wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Bergen cha Norway walikutana na sisi (MUHAS) kujadili jinsi muziki unavyoweza kusaidia kupunguza maumivu ya misuli na mifupa, matatizo yanayoathiri wafanyakazi wengi.

"Katika kikao hicho, wataalamu walisisitiza kuwa maumivu hayo yanahusishwa na kupungua kwa tija kazini na kusababisha kuwa na likizo nyingi za ugonjwa.

"Tunahitaji kuanza utafiti kuona kama kiwango kilichowekwa na WHO, kinaweza kuwa sahihi kwa nchi yetu," alisema.

Aliongeza kuwa wanapanga kufanya utafiti zaidi kuhusu matumizi ya muziki kazini, si tu kwa wagonjwa bali pia kwa wafanyakazi wenye afya, alidai mbinu hiyo itawasaidia kuelewa jinsi muziki unavyoweza kuboresha afya na ustawi wa wafanyakazi na kuongeza kuwa wapo kwenye mchakato wa kujadili namna ya kupata ufadhili wa mradi huo wa kiutafiti ambao ni muhimu kwa afya ya wafanyakazi nchini.

 Alisema kuwa timu ya watafiti kutoka Bergen na Ethiopia wakati wa mkutano wa NORHED II, ilitembelea Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambayo imekuwa Kituo cha Ubora cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kujionea namna sanaa za maonesho zinavyoweza kutumia muziki katika nyanja mbalimbali.

 Alisema kuna fursa ya kuboresha ushirikiano baina ya TaSUBa na Idara ya Muziki ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuona namna muziki tiba unaweza kutumika mahali pa kazi bila kuathiri uzalishaji na mfumo wa kazi na ajira.