Mbu mpya ‘Stephie’ tishio la mapambano dhidi ya malaria

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 11:46 AM Oct 25 2024
Mbu mpya ‘Stephie’
Picha: Mtandao
Mbu mpya ‘Stephie’

WAKATI dunia ikitarajia kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa wa malaria ifikapo mwaka 2030, tishio la kibaolojia na mabadiliko ya tabianchi limeibuka.

Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya, Dk. Samwel Lazaro, alisema hayo jana kuhusu hatua iliyopigwa na nchi, kupitia kituo cha redio cha Clouds FM kwamba mbu aina ya ‘Anopheles stephensi’, maarufu ‘stephe’ hadhibitiki kwa viuatilifu vilivyoko.

Alisema taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2023 inaeleza duniani kulikuwa na ongezeko la zaidi ya wagonjwa milioni tano kipindi cha mwaka 2022, ikilinganishwa na wagonjwa wa malaria kwa mwaka 2021. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwaka 2022 kulikuwa na wagonjwa milioni 249 kulinganisha na wagonjwa milioni 244 mwaka uliopita. Hata hivyo, taarifa hiyo inaonyesha kuwa vifo vitokanavyo na malaria vilipungua kutoka 610,000 mwaka 2021 hadi 608,000 mwaka 2022.  

“Duniani nchi 44 zimeshatokomeza ugonjwa huo, zikiwamo nne kutoka Afrika ambazo ni Cape Verde, Mauritius na Morocco na baadhi zikiwa kwenye hatua ya kufikia lengo hilo miaka mitano ijayo kutoka sasa.

“Kuna matishio ambayo yameibuka sasa, kabla ya wakati ambao malengo yalikuwa yanawekwa hayakuweko. Duniani kuna mbu aina mpya alianzia Asia Mashariki na amekuwa akionekana katika nchi mbalimbali, kwanza ameshindwa kudhibitika na viuatilifu tunavyovitumia sasa hivi.

“Pia mbu huyu uwezo wake wa kuambukiza malaria ni mkubwa kuliko mbu tuliokuwa nao awali, kwa miaka yote na sasa mikakati inaelekea katika kumdhibiti,” alisema Dk. Lazaro.

Alisema kuna hatua mbalimbali na kila nchi ina mikakati yake katika kutekeleza malengo na kwa Tanzania imejiwekea miaka mitano katika mipango kwa sababu nchi ni kubwa na iko mikao tisa ambayo ina kiwango cha chini ya asilimia moja.

“Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Mwanza, Songwe, Iringa na Dar es Salaam, ina kiwango cha asilimia moja cha malaria. Kwa mujibu wa utafiti wa NBS mwaka 2022, kiwango cha malaria ni asilimia 8.1 nchini lakini baadhi ya mikoa kiwango kiko juu,” alisema.

“Kiwango kiko juu ikiongozwa na mkoa wa Tabora ambako kuna asilimia 23.4, ikifuatiwa na Mtwara (20), Kagera (18), Shinyanga  (16) na Mara (15) wakati Geita na Kigoma ni asilimia 13,” aliongeza. 

WHO inaeleza kuwa ifikapo mwaka 2030 lengo ni kupunguza maambukizi ya malaria angalau kwa asilimia 90 na kupunguza viwango vya vifo vya ugonjwa huo kwa asilimia  90.

Kadhalika, lengo ni nchi kuondoa malaria kwa nchi 35 ifikapo 2030 na kuzuia kuzuka tena kwa malaria katika nchi zote ambazo hazina malaria.

Kanda ya Afrika inabeba sehemu kubwa isiyo na mzigo wa malaria duniani. Mwaka 2022, eneo la Afrika lilikuwa na asilimia 94 ya wagonjwa wa malaria (milioni 233) na asilimia 95 (580,000) ya vifo vya malaria.

Aidha, watoto walio chini ya miaka mitano walichangia takriban asilimia 80 ya vifo vyote vya malaria katika eneo la Afrika, kwa mujibu wa WHO.

Kundi la watoto wachanga, watoto chini ya miaka mitano, wajawazito, wasafiri na watu wenye Virusi Vya Ukimwi (VVU) au UKIMWI wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa malaria.

Nchi nne za Afrika zilichangia zaidi ya nusu ya vifo vyote vya malaria duniani kote, Nigeria asilimia 26.8, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) asilimia 12.3, Uganda (5.1) na Msumbiji (4.2).

Katika karne ya 20 pekee, malaria iliua kati ya watu milioni 150 na milioni 300, ikichukua asilimia mbili hadi tano ya vifo vyote (ripoti ya Carter na Mendis, 2002).

Wanaougua ugonjwa huo wengi ni kutoka nchi maskini zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara, Asia, bonde la Amazon na maeneo mengine ya kitropiki, asilimia 40 ya wakazi wa dunia, bado wanaishi katika maeneo ambayo malaria unakosambaa.