Tanzania yajipambanua matumizi sahihi ya teknolojia kukabili maafa

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 07:33 PM Oct 25 2024
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga (kushoto) akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum na Mwakilishi wa kundi la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Neema Lugangira wakati wa Mkutano huo.
Picha: Ofisi ya Waziri Mkuu
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga (kushoto) akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum na Mwakilishi wa kundi la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Neema Lugangira wakati wa Mkutano huo.

TANZANIA imeendelea kuonesha umahiri wake katika masuala ya menejimenti ya maafa kwa kuzingatia mifumo sahihi ya kukabiliana na majanga na matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na miongozo, kanuni na sheria zinazoongoza katika uratibu wa masuala hayo.

Hayo yameelezwa leo nchini Namibia na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga, wakati akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Viongozi kuhusu masuala ya kupunguza athari za maafa.
 
Ameeleza kuwa uwekezaji mkubwa umefanywa na Serikali ya Tanzania hususani katika kuhakikisha teknolojia inavusha Taifa kwenye kukabili maafa ambako ilianzisha Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura.
 
“Kituo hicho kimeifanya nchi kuwa mahiri katika masuala ya menejimenti ya maafa hususan katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea,” amesema Ummy.
 
Akizungumzia mkakati wa miaka kumi wa Nishati safi ya kupikia ambao utekelezaji wake umeanza mwaka huu hadi 2034, ameeleza kuwa unalenga kuhifadhi mazingira, kulinda afya kwa kuzuia matumizi ya kuni na mkaa ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabia nchi.
 
“Suala la mabadiliko ya tabia nchi linaathiriwa na ukataji miti inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kuchagiza ukosefu wa mvua za kutosha, na uwepo wa ukame unaoathiri uzalishaji wa chakula, na tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua mkakati huo,” amesema Ummy.
 
Amesema moja ya mikakati ambayo Tanzania imejiwekea ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.
 
"Kama nchi tumejipanga kuhakikisha taasisi za serikali na mashirika binafsi yanawekeza ipasavyo katika matumizi ya nishati safi kwa maslahi mapana ya mazingira safi na salama, afya zetu na Afrika kwa ujumla,” amesema Ummy.
 
Pia ametoa wito kwa mataifa mbalimbali duniani kufuata nyayo za Tanzania kwa kuhakikisha zinaweka mikakati madhubuti ya muda mfupi na mrefu ya Nishati safi ya Kupikia ili kuifanya Dunia kuwe mahali safi na salama pa kuishi.