Wananchi Kata ya Makuro warahisishiwa mawasiliano ya simu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:17 PM Oct 26 2024


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa.
Picha:Mpigapicha Wetu
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema, wananchi takriban 15,613 wa Kata ya Makuro na maeneo ya jirani wataanza kupata huduma ya mawasiliano ya simu ya uhakika kutokana na kukamilika ujenzi wa mnara wa mawasiliano.

Mnara huo umejengwa na kampuni ya Airtel kupitia ruzuku ya serikali iliyotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ya kiasi cha sh. milioni 115.

Waziri Silaa ameyasema hayo, wakati wa uzinduzi wa mnara huo uliojengwa katika kijiji cha Mikuyu, Kata ya Makuro wilaya ya Singida Mkoani Singida, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi kutembelea, kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika Mkoa wa Singida.

Akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema, awali mnara huo ulikuwa unatoa huduma kwa teknolojia ya 2G pekee ambayo huwezesha watumiaji kuwasiliana kwa kupiga simu za sauti na kutuma ujumbe mfupi yaani SMS tu, lakini kuanzia  Oktoba 24, 2024 mnara huo uliongezewa teknolojia ya 3G na 4G ili kuwezesha matumizi ya huduma za mtandao wa intaneti kupitia simu na vifaa vingine.