Hatua zichukuliwe kuwaokoa watoto katika majanga haya

Nipashe
Published at 08:13 AM Oct 27 2024
Hatua zichukuliwe kuwaokoa   watoto katika majanga haya
Picha;Mtandao
Hatua zichukuliwe kuwaokoa watoto katika majanga haya

KATIKA ukurasa wa ne wa gazeti hili, kuna ripoti maalum inayoeleza kuzagaa kwa watoto kwenye migahawa ya mamalishe katika miji mbalimbali, huku Manispaa ya Tabora na jiji la Mwanza ikiwa mfano.

Watoto hao si kwamba hawana wazazi bali ni wa mamalishe hao ambao wamedai kuwa wanakwenda nao katika maeneo ya kujipatia riziki kutokana na kukosa wasichana wa kuwaachia. Kutokana na sababu hiyo, wameeleza kuwa suluhisho waliloliona ni kwenda nao katika shughuli za kila siku. 

Licha ya sababu hiyo, mamalishe hao wamesema wanalazimika kufanya hivyo, kwa sababu ya hali ya kipato chao kushindwa kuajiri watumishi wa ndani kwa ajili ya kulea watoto hao. Pia mmoja amesema sababu ya kufanya hivyo ni kutokana na mwenza wake kushindwa kuwajibika kwa matunzo ya familia na kwamba yeye ndiye mtafuta riziki ndani ya ndoa yao. 

Picha zilizopigwa katika maeneo hayo zinaonesha kuwa mazingira wanayokuwa  watoto hao katika migahawa ya mamalishe si rafiki, kwa makuzi yao wala afya kwa ujumla. Watoto hao wameonekana wakichambua mboga, wakicheza katika maeneo hatarishi yakiwamo maegesho ya magari.  

Kulingana na mazingira hayo, watoto hao ni rahisi kuchukua tabia na matendo yanayofanyika kwenye maeneo hayo kama vile matusi na udhalilishaji. 

Kwa mantiki hiyo, kama inavyofahamika, kuna uwezekano mkubwa mustakabali wa watoto hao ukawa mbaya kwa kuwa mtoto ana tabia ya kunakili, kuiga na kuchukua kila kitu kinachofanyika katika mazingira husika. Kwa hiyo, kuna uwezekano mkubwa watoto hao wakajikuta wanakua na kuishi katika mazingira ya matusi, huku wakishuhudia kauli chafu kutoka kwa wateja wa mama zao. 

Baadhi ya viongozi, wakiwamo watendaji wa kata na mitaa,  wamekiri kufahamu vitendo hivyo na kwamba wanatarajia kuchukua hatua dhidi ya wazazi, ili kuwalinda watoto na mazingira magumu waliyomo. Lakini jambo la kujiuliza walikuwa wapi mpaka kutamka kuwa wnatarajia kuchukua hatua ilhali jambo hilo limeshaota mizizi? 

Ni dhahiri kwamba kwa muda ambao watoto hao wameshakaa  katika mazingira hayo, tayari kuna athari za kisaikolojia, kiafya na makuzi ambazo wameshazipata. Pamoja na hayo, kama waswahili wasemavyo kawia ufike, bado kuna nafasi ya kuwaokoa watoto hao dhidi ya majanga yanayoweza kuendelea kuwakumba kama wataendelea kuwamo katika mazingira hayo. 

Serikali za mitaa, kupitia watendaji wa kata na mitaa pamoja na wataalamu wa elimu, afya na mazingira, wanapaswa kuchukua hatua za haraka kuwanusuru watoto hao, ambao miaka mingi wamekuwa wakitajwa kuwa ndio taifa la kesho. Mpango mmojawapo unaoweza kufanyika ni kuwapeleka katika shule za awali zilizo karibu na mamalishe hao na kuchukuliwa, baada ya mama zao kumaliza shughuli zao. 

Njia nyingine inayoweza kuchukuliwa na kuwanusuru ni kuweka sheria ndogo katika mamlaka za serikali za mitaa zitakazowazuia wazazi kwenda na watoto wao kwenye shughuli zao za kujipatia riziki kama vile migahawa ya mamalishe. Aidha, iko sheria inayomlinda mtoto, hivyo nayo inapaswa kutumika, ili watoto  hao waokolewe dhidi ya madhila yanayowanyemelea. 

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mzazi atakayemweka mtoto katika mazingira hatarishi anaweza kufikishwa mbele ya sheria na kutozwa faini au kifungo, au kupewa adhabu zote kwa pamoja. 

Ni imani kwamba kama sheria hizo zitatekelezwa, kutakuwa na fundisho kubwa dhidi ya wazazi kama hao na wakati huo huo, watoto kuokolewa kwenye majanga yanayowakabili.