Serikali kuunda timu maalum kurejesha huduma za vivuko mafia

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 09:30 PM Oct 26 2024
 Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.

SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Ulinzi na imesema itaunda timu maalum itakayoshughulikia na kusimamia urejeshaji wa huduma ya usafiri wa Vivuko katika Wilaya ya Mafia.

Vivuko vya MV Kilindoni na MV Songosongo vinavyofanya safari kati ya kituo cha Mafia - Nyamisati (Kibiti) vilivyosimamisha huduma ya usafiri tangu  Oktoba 10, 2024.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wilayani Mafia mkoani Pwani wakati akikagua matengenezo ya Kivuko cha MV Songosongo kinachosimamiwa na Jeshi la Wananchi kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa leo Oktoba 26, 2024 

Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa huduma ya usafiri wa vivuko katika Wilaya ya Mafia ambayo imesimama kutoka na vivuko vya MV Kilindoni na MV Songosongo kupata hitilafu ambapo sasa kazi ya matengenezo inaendelea kwa vivuko vyote wiwili.

“Serikali ipo kazini, na kupitia timu hii kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani itafanya jitihada za haraka za kurudisha huduma za vivuko viwili vya MV Songosongo na MV Kilindoni ili kuwaondolea adha wana Mafia ya kukosa usafiri wa Vivuko”, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa amesema kuwa Mkakati wa Serikali ni kuongeza kivuko kingine ili kusaidia wakati wa dharura kwa kutoa huduma kwa wananchi pindi kivuko kingine kinapopata hitilafu.

Aidha, Bashungwa amewahakikishia Wananchi wa mafia kuwa Timu hiyo ya Wataalam itafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanarejesha huduma za vivuko haraka iwezekanavyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema Ofisi yake inaendelea kuongea na Wawekezaji wa Sekta binafsi watakaoweza kufanya uwekezaji wa huduma ya Usafiri na Hoteli ili kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma hizo ambazo zitaendelea kufungua uchumi wa Wilaya ya Mafia.