CHADEMA yakanusha uvumi kutoshiriki uchanguzi mitaa

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 08:32 AM Oct 27 2024
Spika wa Bunge la Wananchi wa CHADEMA, Suzan Lyimo.
Picha: Mtandao
Spika wa Bunge la Wananchi wa CHADEMA, Suzan Lyimo.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekanusha taarifa zilizosanmbaa mtandaoni kuwa kimejitoa katika Uchaguzi Serikali za Mitaa na kusisitiza hakina mpango huo.

Sambamba na kuweka msimamo huo, chama hicho kimesema kimejipanga vizuri kushiriki na kushinda katika uchaguzi huo.

Jana, chama hicho kilianza kutoa fomu za serikali kwa wanachama wake walioteuliwa nchi nzima za kugombea nafasi mbalimbali waliozoteuliwa na chama.

Akizungumza jana na vyombo vya habari kuhusu uchaguzi huo, Spika wa Bunge la Wananchi wa CHADEMA, Suzan Lyimo, alisema chama hicho hakijajitoa katika kinyang’anyiro hicho kama uzushi uliosambaa mtandaoni.

Juzi, Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, kupitia taarifa yao kwa umma, alisema hawajajitoa na wala hawana mpango wa kujitoa kwa sasa.

“Tunawahimiza wanachama wetu walioteuliwa nchi nzima kesho (jana) wajitokeze mapema kwenda kuchukua fomu za serikali za kugombea nafasi mbalimbali walizoteuliwa na chama,” alisema.

Mrema alisema taarifa ya picha mjongeo iliyosambaa mitandaoni yenye maudhui kuwa CHADEMA imejitoa katika uchaguzi 2024, ni za uongo, uzushi na za kupuuzwa.

Katika mkutano huo, Lyimo aliendelea kusisitiza madai kwamba wameshuhudia mawakala kuzuia kupata takwimu za waandikishwaji na baadhi wakipingwa na wanafunzi chini ya miaka 18 wakishangaa kuandikwa.

Mwachumu Kadutu, Msemaji wa CHADEMA Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwenye Bunge la Wananchi, alisema upungufu waliouona katika mchakato uliofanyika kwa siku 10 hadi ubandikaji majina ni pamoja na waliyoona kwenye daftari lenyewe haviulizi ni raia wa wapi.

Alisema kilichofanyika ni mtu kuulizwa majina matatu, umri na kutia saini, kwamba hali hiyo inafungua mwanya hasa kwa mipakani wasio raia kushiriki mchakato huo.

“Haliulizi unakaa mtaa gani, inatoa mwanya kwa watu kutoka mtaa mwingine kwenda mwingine kupiga kura. Umri umetajwa miaka 18 kuendelea, lakini utathibitishaje kama ana umri huo? Ikitokea utamzuia,” alihoji.

Alisisitiza madai kwamba wameshuhudia mapungufu ya wanafunzi kuandikishwa walio chini ya miaka 18 wakati kanuni inasema ni miaka 18 kuendelea.

“Vituo vingi vipo shule za sekondari, kwa kidato cha kwanza hadi kidato cha nne wameandikishwa, ukipiga hesabu mtoto mwenye umri wa miaka saba ambaye yupo kidato cha nne maana yake hajafikia kigezo cha kuandikishwa.

“CHADEMA tunaomba turuhusiwe kupiga kampeni shuleni wanahaki ya kusikiliza sera zetu kwa sababu wana haki ya kupiga kura, ili wanapochagua wachague kwa kusikia na kuona wagombea na kuelewa sera zao,” alisema.