UCHAGUZI UJAO: IGP atoa onyo wavurugaji amani

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 08:15 AM Oct 27 2024
Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP) Camilus Wambura
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP) Camilus Wambura

JESHI la Polisi Nchini limesema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani, halitavumilia mtu au kikundi cha watu kitakachovunja sheria kwa kisingizio chochote.

Limesema hatua za kisheria zitachukuliwa, ili jamii iendelee kuishi kwa amani na kutimiza haki ya kikatiba kushiriki uchaguzi huo.

Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP) Camilus Wambura, aliyasema hayo jana wakati akifunga Mafunzo ya Awali ya Polisi Kozi Namba Moja ya Mwaka 2023/24 yaliyofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania (CCP), Moshi mkoani  Kilimanjaro.

IGP Wambura alisema Jeshi la Polisi pamoja na kutekeleza majukumu yake, lina wajibu wa kuhakikisha amani na utulivu vinatamalaki na askari wote wanadumisha amani na uzalendo kwa taifa, kwa kusimamia sheria na kanuni za uchaguzi.

“Tuwapinge wote wenye nia mbaya wasioitakia mema Tanzania. Tuwapinge  wote wenye nia mbaya wanaoshabikia uhalifu au vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo vingi vinachochewa na itikadi za siasa chafu, kwa maslahi ya watu wachache walio katika jamii zetu,” alisema.

IGP Wambura alisisitiza kuwa nchi iko salama na kwa kushirikiana na Watanzania wanadumisha amani, ili taifa kuwa kisiwa cha amani na kimbilio la wageni wote duniani.

Alisema wanaendelea kukabiliana na uhalifu wa kisasa kama vile uhalifu wa kupanga na unaovuka mipaka, ikiwamo biashara haramu usafirishaji binadamu, uhalifu mitandaoni na utakatishaji fedha. 

“Uhalifu huu kwa kiasi kikubwa umetokana na utandawazi unaochagizwa na kasi ya ukuaji wa teknolojia. Vilevile, kama jamii tunakabiliwa na uhalifu unatokana na mmomonyoko wa maadili, ikiwamo kuendekeza mila na desturi potofu, unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto,” alisema.

Wambura alisema nchi imeendelea kukumbwa na mauaji kutokana na wivu mapenzi, kujichukulia sheria mkononi na kulipiza kisasi.

Alisema kutokana na changamoto hizo, Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada za kubuni miradi mipya ya Polisi Jamii yenye dhumuni la kutokomeza mazalia na visababishi vya uhalifu kuanzia ngazi ya familia.

“Serikali imeendelea kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ya kukabiliana na uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka, ikiwamo kudhibiti usalama wa mifumo ya kieletroniki na kudhibiti mipaka kwa mifumo ya kisasa ya kieletroniki na ongezeko kubwa la magari maalumu ya doria.

“Siri ya kutokomeza uhalifu ni kupanda mbegu wema ndani ya jamii na kuweka mikakati thabiti na shirikishi ya kukabili changamoto iliyoko na tumejipanga na tunaendelea kutoa elimu,” alisisitiza.

IGP Wambura aliuhakikishia umma kuwa, wako imara na wametanua wigo wa ushirikiano na taasisi za serikali na zisizo za serikali, vyombo vya dini, wanasiasa na asasi za kiraia.

“Kidole kimoja hakivunji chawa. Mwanzilishi wa Jeshi la Polisi la kisasa alisema ‘polisi ni jamii na jamii ni polisi’ akimaanisha kila mwanajamii anao wajibu kushiriki katika juhudi za kushughulikia uhalifu na kuhakikisha amani na utulivu vinatamalaki katika taifa,” alisema.

IGP Wambura alisema, ili kupunguza mzigo Jeshi la Polisi wa kupambana na uhalifu, wazazi na walezi hawana budi kuwalea watoto wao katika njia iwapasayo kwa kuwa uhalifu huanzia kwenye ngazi ya familia.

Kuhusu mafunzo hayo, alisema yamewajengea uwezo askari polisi wa kufanya kazi kwa weledi, ukakamavu na msisitizo wa nidhamu kwenye shughuli za polisi. Alisema shule imewafundisha na kuwachuja vizuri na sasa wanawapeleka vituoni kufanya kazi.

“Ili kutimiza vyema malengo ya kazi na kulinda raia na mali zao mkayaishi mliyofundishwa na kusimamia haki, kutenda kwa weledi na kuwa waadilifu na mkaishi kiapo mlichoapa na kutoa huduma bora kwa mteja,” alisisitiza.