Wafurahia faida nono mauzo ya korosho

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:44 PM Dec 27 2024
Wafurahia faida nono mauzo ya korosho
Picha:Mtandao
Wafurahia faida nono mauzo ya korosho

WAKULIMA wa korosho wa Chama Kikuu cha Ushirika Masasi-Mtwara na Nanyumbu (MAMCU), kwa kauli moja wamekubali kuuza korosho tani 579 kwa bei ya juu ya Sh. 2,140 na bei ya chini ya Sh. 1,810.

Korosho hizo zimeuzwa mwishoni mwa wiki iliyopita  katika mnada wa 11 wa korosho ulioendeshwa kwa mfumo wa soko la bidhaa Tanzania (TMX) katika kijiji cha Mpapura mkoani Mtwara na kuhudhuriwa na mamia ya wakulima wa zao hilo. 

Wakizungumza baada ya kumalizika kwa mnada huo, viwanja vya  Chama cha Msingi Mpapura ( AMCOS) wakulima hao walisema katika msimu huu zao hilo limekuwa na bei nzuri tofauti na misimu iliyopita. 

Ally Mohamed, mkulima kijiji cha Mpupara, alisema bei za korosho zimeendelea kuwa za kuridhisha kwa wakulima tangu minada ya korosho ilipoanza Oktoba, mwaka huu. 

Alisema kwa bei zilizoko sokoni zinazojitokeza kwenye minada kwa sasa, wanaendelea kuishukuru serikali kwa kuwa imewaheshimisha wakulima wa korosho hasa mikoa ya kusini. 

 Asha Juma ambaye pia ni mkulima, alisema kupitia bei hizo za korosho msimu huu,  amepata fedha za kutosha baada ya kuuza zaidi ya tani sita na kwamba fedha hizo zimemsaidia kujenga nyumba ya kuishi na familia yake. 

"Tunaipongeza serikali hasa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ametuheshimisha sisi wakulima kwa sababu bei ya korosho imekuwa ya kuridhisha msimu huu, tumepata maendeleo mazuri," alisema Juma.  

Alisema  kama serikali itaendelea kulinda thamani ya korosho, wakulima watakuwa na maendeleo makubwa ikilinganishwa na misimu ya miaka ya nyuma ambapo walikuwa wakilima na kutopata manufaa yoyote yale. 

Fadhili Salumu, mkulima kijiji cha Libobe mkoani Mtwara, alisema  wanafurahishwa na bei hizo, hivyo kupitia mnada wa 11 wanaridhia kuuza korosho zao tani 579 bei ya juu ya Sh. 2,140 na bei ya chini Sh. 1,860.  

 Mmwenyekiti wa MAMCU, Azam Julajula, alisema hadi sasa jumla ya minada 11 imefanyika na wakulima wamepata zaidi ya Sh. bilioni 365  za malipo ya minada 10 kati ya hiyo 11 ilifanywa ndani ya msimu huu wa korosho mwaka 2024/25

  Alisema katika minada hiyo, zaidi ya tani 115,000 za korosho za chama hicho,  zimeuzwa na wakulima kupokea malipo yao kwa wakati.