Wafugaji wadaiwa kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 08:34 AM Jul 23 2024
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli.

BAADHI ya wafugaji wilayani Mvomero, mkoani Morogoro wamebuni mbinu mpya ya kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima kwa kuingiza mifugo shambani usiku.

Kutokana na hatua hiyo, uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi umeweka mkakati wa kuendesha doria za usiku kwa kushirikiana na wananchi ili kudhibiti kadhia hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya kukamatwa kwa ng'ombe 20 wanaodaiwa wa mfugaji Taifa China, mkazi wa Dakawa, wilayani Mvomero wakiwa wameingizwa katika mashamba ya wananchi Julai 21, mwaka huu.

Mbali na mashamba ya wananchi, mifugo hiyo pia inadaiwa kuingizwa katika mashamba ya umwagiliaji yanayomilikiwa na Ushirika wa Wakulima wa Mpunga Dakawa (UWAWAKUDA) na mashamba ya mahindi katika bloku namba 19.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli, alifika katika eneo hilo jana na kukemea hali hiyo, akitaka hatua za makusudi kuchukuliwa na polisi dhidi ya mtuhumiwa, ili iwe fundisho kwa wenye tabia ya aina hiyo.

Alisema kitendo cha wafugaji kutodhibiti mifugo yao na kuiacha kuzagaa kwenye mashamba ya wakulima nyakati za usiku, hakitofumbiwa macho kwa kuwa kinachochea ukosefu wa utu na ubinadamu na kurudisha nyuma maendeleo ya wengine ambao wanatumia nguvu na gharama kubwa kustawisha mazao yao.

Aliagiza kuwe na doria  za kila mara kusaka mifugo inayorandaranda nyakati za usiku na itakayokamatwa ipelekewe ombi maalum mahakamani ili hakimu atoe kibali cha kutaifishwa.

"Huku kutozwa faini kila siku wanachukulia ni jambo jepesi na inawapa kiburi, na kwa vile wana fedha, wanaona ni kawaida tu, wanalipa na kulisha tena kwa mara nyingine, sasa ifike mahali hili la faini liishe na lije la kutaifisha mifugo," alionya Mkuu wa Wilaya.

Alitoa siku tatu kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa kushirikiana na polisi kuondoa kambi za mifugo jirani na skimu hiyo ya umwagiliaji, sambamba na mifugo katika maeneo ambayo hayakutengwa kwa shughuli za ufugaji.

Mwenyekiti wa UWAWAKUDA, Charles Pangapanga alisema kwa kipindi kirefu wamekuwa na changamoto ya wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima, pia wafugaji kuweka kambi jirani na mashamba hayo.

Alisema awali kulikuwa na maridhiano baina ya wakulima na wafugaji kwamba kila mmoja aheshimu maeneo ya mwenzake kwa lengo la kudhibiti mifugo isiingie katika mashamba ya wakulima.

Alisema pamoja na maridhiano hayo, bado wafugaji wamekuwa wakikiuka na kuleta usumbufu mkubwa na wa mara kwa mara kwa kuingiza mifugo katika mashamba ya ushirika ambayo kwa umoja wake yana ukubwa wa ekari 5,000.

"Eneo hili lina hati miliki na miundombinu ya skimu ya umwagiliaji na kusababisha hasara kwa wakulima ambao wanatumia nguvu na gharama kubwa kuendesha kilimo, lakini skimu za umwagiliaji zina miundombinu ambayo haipaswi kuharibiwa kwa sababu ndiyo inayosaidia kumwagilia na kuhamisha maji upande mmoja kwenda mwingine," alisema Pangapanga.

Wakulima wengine, Michael Sylvester, Salum Sekwao, Seleman Nassoro na Christina Juma, wote wa Dakawa, kwa nyakati tofauti walisema uingiaji holela wa mifugo shambani unasababisha hasara kubwa.

Mfugaji Taifa China ambaye ng'ombe 20 wamekamatwa kwa tuhuma za kuingia katika mashamba ya wakulima, alidai mifugo yake ilivunja zizi usiku na kuingia katika mashamba ya wakulima.