Treni ya umeme Dar-Dodoma kumekucha

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:54 AM Jul 23 2024
Treni ya umeme.

SERIKALI imesema ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma umekamilika kwa asilimia 99, huku safari za treni zikitarajiwa kuanza kesho.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini hapa, Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema hivi sasa wanaendelea kukamilisha vitu vichache ili ifikapo Julai 25, mwaka huu safari zianze rasmi.

"Hivi sasa tumefikia asilimia 99 na wataalamu wetu wanamalizia vitu vichache ili safari zianze rasmi siku ya Alhamisi Julai 25 mwaka huu. Tumeweka utaratibu mzuri kwa wananchi kukata tiketi kwa njia ya mtandao ili kurahisisha mambo.

"Baada ya kukamilisha kazi zote, wizara inaendelea kuweka utaratibu ili Rais Dk. Samia aweke jiwe la msingi la kuzindua rasmi safari za treni ya mwendo kasi," alisema.

Kadogosa aliomba viongozi wa kimila kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji miundombinu ya SGR kwa kuwa serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia ujenzi wake.

"Viongozi wa kimila, wakiwamo machifu, ni muhimu hasa katika ulinzi wa miundombinu ya reli. Niendelee kuwaomba ndugu zetu mwendelee kutoa elimu kwa wananchi faida ya reli hii hasa katika kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla," alisema.

Chifu wa Dodoma, Mazengo wa Pili, alipongeza serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati, ukiwamo ujenzi wa reli hiyo ambao kukamilika kwake kutafungua nchi kiuchumi.

Alisisitiza wananchi wanaozunguka miradi mikubwa ya kimkakati kuendelea kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo yao kujikwamua kiuchumi.