Tanzania yapaa kwa huduma mawasiliano

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 06:57 AM Apr 27 2024
 Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi.

TANZANIA imekuwa na maendeleo makubwa ya huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu, kwa mijini na vijijini kwa kufanikisha kutoa laini za simu milioni 72.5 hadi kufikia Machi mwaka huu.

Vilevile, katika kipindi hicho idadi ya watumiaji wa mitandao ya Intaneti imekua hadi kufikia watu milioni 36.8

 Hayo aliyasema jana jijini Arusha Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, alipokuwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana na Tekniolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

 "Idadi kubwa ya watanzania wa mijini na vijijini imefikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu na mitandao ya Internet, haya ni maendeleo makubwa katika sekta ya mawasiliano hapa nchini,"alisema.

 Alisema idadi hiyo ni kubwa kufikiwa katika utoaji wa huduma hizo, ukilinganisha na nchi zingine.

 Pia alisema upatikanaji wa huduma hizo kumewezesha jamii ya watanzania kushirikia ipasavyo uchumi wa kidijiti.

 "Mazingira haya ya upatikanani wa huduma hizi yanawezesha  upatikanaji wa huduma za kijamii kwa urahisi na kusaidia kuzalisha ajira na  kufungua fursa mbalimbali mpya kwenye kilimo na maeneo mengine, kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kiuchumi," alisema

 Pia aliagiza vyuo vikuu,ya kati,shule za sekondari na Msingi kuanzisha klabu za kidijiti ili kuhamasisha  wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi nabkukuza ujuzi wa kidijiti.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TRCA), Dk. Jabir Bakari, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha wasichana kuchukua masomo ya sayansi, uhandisi, teknlojia na hisabati na kuwawezesha na kuwaandaa kuja kunufaika na fursa zilizopo,yakiongozwa na kaulimbiu isemayo 'Uongozi.'

 "Maendeleo ya dunia ya sasa yameshikiliwa sana na matumizi ya teknolojia katika kila nyanja hivyo ni muhimu wasichana kujikita katika utengenezaji wa mifumo na programu za kiteknolojia, kusoma masomo ya uhandisi,kujikita katika tafiti mpya kama vile akili bandia na kuwa sehemu ya utaalam wa masomo ya Tehama kwa ngazi za elimu na pia kuja kushiriki katika ngazi ya kutunga sera,hasa katika eneo hili la TEHAMA,” alisema.

 Sekta ya mawasiliano ya simu nchini, alisema  imeendelea kukua kwa kasi ambapo hadi Machi mwaka huu laini za simu zilikuwepo milioni 72.5  toka laini laini milioni 64.1  Juni, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 13. 

Alisema takwimu hizo za Machi zimeonyesha ongezeko la watumiaji wa intaneti kwa asilimia 8.2 toka watumiaji  milioni 34 juni mwaka jana hadi kufikia watumiaji milioni 36.8. 

"Sababu zilizochangia ongezeko hilo ni matumizi ya intaneti,ambayo yamechangia kuwa na maudhui mengi ya kiswahili,uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu iliyofanyika kwenye maeneo mbalimbali,simujanja zimeongezeka kutoka milioni 16.7  Juni 2023, hadi milioni 20.1,Machi mwaka huu ikiwa ni ongezeko la asilimia 20,"alisema.