OFISA Mwandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Carol Makundi amesema Watanzania wengi wamekuwa wakihofia kutumia umeme kama nishati ya kupikia kwa kudhani kuwa gharama zake ni kubwa, huku akibainisha kuwa kupika Maharage kwa kutumia umeme gharama yake ni Sh 200 pekee.
Carol ameyabainosha hayo jana Jumamosi, Januari 11, 2025 katika hafla maalumu ya uhamasishaji na kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia kwa viongozi wa dini ya Kiislam Jijini Arusha ambayo imeratibiwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo.
Carol ameeleza kuwa umeme sio tu nishati rahisi na salama bali pia ni suluhisho endelevu kwa changamoto za kupikia nchini.
"Matumizi ya umeme katika kupikia yanaweza kusaidia kupunguza gharama za maisha, kulinda mazingira, na kuboresha afya za wananchi," amesema Carol.
"Matumizi ya umeme yanaweza kushusha gharama kwani nusu kilo ya Maharage kupikia kwa umeme inagharimu hadi Sh 200 pekee, ikilinganishwa na 1,200 kwa mkaa, 800 kwa gesi, na 600 kwa mafuta ya taa," amesema Carol.
Amesema kuwa kupikia kwa umeme si tu nafuu bali pia kuna mchango mkubwa katika jitihada za kupunguza uzalishaji wa kaboni na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.
Pia TANESCO imeeleza mikakati yake ya kukuza matumizi ya nishati safi nchini, ikiwemo kutoa elimu kwa watumiaji wa kawaida, viongozi wa dini, na wadau wengine kuhusu faida za kupikia kwa umeme.
Kwa mujibu wa Carol, shirika hilo limekuwa likifanya tafiti kubaini vifaa bora vya kupikia vinavyotumia umeme kidogo ili kupunguza gharama za awali kwa watumiaji, huku likishirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wizara ya Nishati katika kusukuma mbele ajenda ya nishati safi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED