Rais Samia, Mwinyi ponyeni makovu ya Mapinduzi kumaliza siasa za uhasama

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:51 AM Jan 12 2025
Rais Samia, Mwinyi ponyeni makovu ya  Mapinduzi kumaliza siasa za uhasama.
Picha:Mtandao
Rais Samia, Mwinyi ponyeni makovu ya Mapinduzi kumaliza siasa za uhasama.

LEO Januari 12, imedondokea siku ile ya Januari 12, 1964. Ilikuwa ni siku ya Jumapili kama leo. Katika siku hii, Watanzania wanaadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Wakati Wazanzibari wengi wanasherehekea kuyapongeza Mapinduzi hayo na wengine hadi kuyapa utukufu kwa kuyaita Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, neno  utukufu, ambalo  kwa dini mbili kuu, Wakristo na Waislamu, anayestahili ni  Mwenyenzi Mungu pekee. Kwa hiyo kuita kitu kingine chochote kitukufu ni kama kufuru! 

Kuna  Wazanzibari wengine, japo wachache, siku hii ni siku ya kumbukumbu mbaya, kwa kuwapoteza wapendwa wao kutokana na umwagaji damu wa Mapinduzi hayo na baada ya Mapinduzi. Hakuna ubishi kabisa kuwa Mapinduzi ya Zanzibar, yameleta heri, lakini ni ukweli mchungu pia yalisababisha maumivu makubwa kwa waliopinduliwa ambao wanaishi na makovu ya Mapinduzi. 

Kule kwenye mtandao maarufu kuliko mitandao yote ya kijamii nchini Tanzania, Jamii Forums, shamrashamra za kuisubiria siku hii, zilianza siku nyingi kabla kushamirishwa na Fake News kuwa Sultan mpinduliwa anarejea Zanzibar kufanya ziara rasmi na atahudhuria maadhimisho ya leo.  

Januari 9, 2025, Zanzibar itashuhudia tukio la kihistoria itakapompokea Sultan Jamshid bin Abdullah kurejea kwenye pwani zake.  Hilo la Sultani kurejea mimi nikalidaka na kulitolea mapendekezo yangu 10 kwa SMZ.

 Ndipo kaka yangu mmoja, kutoka Zanzibar, naomba kumtaja kwa jina moja tu Kaka Chalz, ni kaka yangu alinipokea RTD, akatufundisha kazi ya utangazaji, hivyo tunawaheshimu sana kaka zetu hawa, na hata tunapokosea, hawaachi kutupigia simu kuendelea kutuongoza mpaka leo mpaka kesho, Asante Kaka Chale!. 

Basi Kaka Chalz akaniuliza una uhakika na chanzo chako cha habari kuwa hii ni habari ya kweli? Nikamjibu  kwa vile imetangazwa na Jamiiforums, kwa jina maarufu JF, ni chombo cha kuaminika, ingekuwa fake, JF inatumia mfumo wa Jamii Check kubaini ‘fake news’ na kuzifuta, hivyo itakuwa kweli. 

Ndipo nikaipitia ile habari kwa mara ya pili kusoma chanzo nikakuta ni jamaa yuko Oman!  Nikamtafuta  kaka yangu mwingine Zanzibar huyu ni Mzee Salim Said Salim, mwandishi wa siku nyingi, tunamwita jina la Mzee SSS, yeye ana nasaba kidogo na ukoo wa Sultan. Ukitaka  kumtibua SSS, mwambie Mapinduzi Matukufu.  Salim akawapandia kwa simu Oman, familia ya Sultan wakakanusha kuwa ni feki. Asante Mzee SSS.

 Ndipo nikawasiliana na Mkuu Maxence Mello, chapisho langu likaondolewa ila chapisho la msingi halikuondolewa mpaka leo lipo.  Nikamrudia Kaka Chalz, nikamshukuru kwa angalizo lake lakini nikamwambia baadhi ya yale mapendekezo yangu 10, mengine yako hai,  yafanyiwe kazi. Baada ya hii ‘fake news’, jibu la familia ya Sultan alilotoa, ndilo likanijulisha bado kuna watu wana machungu na Mapinduzi yale. Wapoozwe.

 Huu ni mwaka wa uchaguzi na hakuna ubishi siasa za Zanzibar licha ya uwapo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), bado zinaathiriwa na mzimu wa machozi, jasho na damu zilizomwagika na kufukiwa bila kufanyiwa hitima. Kuna  watu wana makovu ya Mapinduzi yale. 

Matokeo  ya baadhi ya uchaguzi Zanzibar ni yale yale ya ule uchaguzi wa mwaka 1963. Mfano mzuri ni uchaguzi wa mwaka 2015, kuna msemo wa Kiingereza unaosema namba haziongopi!. 

 Matokeo ya iliyokuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) yamethibitisha pasina shaka kuwa uchaguzi wa Zanzibar wa 2015, kama usingefutwa, Maalim Seif Sharif Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF) ndiye angelikuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar kwa kutumia kigezo cha matokeo ya uchaguzi wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT). Kule  Zanzibar uchaguzi haukuwa na dosari. 

Katika  uchaguzi huo, mgombea wa UKAWA, Edward Ngoyai Lowassa, alimshinda mgombea wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli. Katika matokeo hayo, Magufuli alipata kura 194,317 sawa na  asilimia 46.5
 na Lowassa kura 211,033 ambazo ni asilimia 50.50, kura  halali zilikuwa 417,882.

Hii maana yake ni kwamba  Zanzibar upinzani unaweza kushinda lakini kwa vile bado kuna machungu ya Mapinduzi, siku upinzani ukishinda Zanzibar, kutaibuka kulipiza kisasi!

 Nashauri mambo yafuatayo;- 

Kwanza, Zanzibar ianzishe tume ya ukweli na maridhiano ili watu waruhusiwe kutoa madukuduku yao. Pili, Desemba 10 iwe siku ya mapumziko ya uhuru wa Zanzibar. Si  lazima iadhimishwe kwa shamrashamra bali naweza kubadili jina ikaitwa Sultan Day.

 Tatu, neno Matukufu kwenye Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar lisiendelee kutumika bali yaitwe tu Mapinduzi ya Zanzibar na vibwagizo Mapinduzi Daima na Tutayalinda kwa gharama yoyote,tuachane nayo ili kuponya wapinga Mapinduzi.

 Nne, falsafa ya 4R za Rais Samia Suluhu Hassan,itumike hadi Zanzibar. Mshindi  wa kweli wa uchaguzi wa Zanzibar atangazwe.

 Nawashauri  Rais Samia na Rais Dk. Hussein Mwinyi kubalini kutibu makovu ya Mapinduzi  ili kuzimaliza siasa za uhasama. Ikitokea  upinzani umeshinda Zanzibar, hakuna haja kufunika kombe mwanaharamu apite. Iwe  ni kupokezana kwa amani na upendo. 

Heri ya Mapinduzi. 

Paskali 

+255 754 270403