Makipa 12 Ligi Kuu Bara wasotea benchi 2024/25

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:24 AM Jan 12 2025
Makipa 12 Ligi Kuu Bara  wasotea benchi 2024/25
Picha:Mtandao
Makipa 12 Ligi Kuu Bara wasotea benchi 2024/25

JUMLA ya magolikipa 12 wanaocheza katika timu za Ligi Kuu Tanzania Bara hawajadaka mechi hata moja hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, imefahamika.

Simba inaongoza kuwa na idadi kubwa ya makipa wake kati ya wanne iliyowasajili hawajasimama langoni hata mchezo mmoja, ikifuatiwa na Kagera Sugar ambayo makipa wake watatu hawajawahi kukaa golini.

Kwa mujibu wa rekodi zetu na za Bodi ya Ligi, makipa hao ni wale waliosajiliwa kuzichezea timu 16 za Ligi Kuu Tanzania Bara ambazo zinapambana kuwania ubingwa unaoshikiliwa na Yanga.

Makipa wa Simba ambao hawajaonja ladha ya kukaa langoni tangu msimu uanze ni Ayoub Lakred raia wa Morocco, Aishi Manula 'Tanzania One', Hussein Abel na Ally Salim.

Kwa upande wa Kagera Sugar, makipa watatu ambao wamekaa benchi mzunguko wote wa kwanza, ni Shija Jackson, Bruno Bruno na Said Kipao.

Katika michezo yote 15 ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyocheza, Simba imemsimamisha langoni, Moussa Camara, ambaye ni raia na Guinea, huku Kagera Sugar ikimtumia Ramadhani Chalamanda katika michezo yote.

Makipa wa Azam FC, ambao mpaka sasa bado hawajakaa langoni ni Ali Ahmada na Hamisi Athumani.

Makipa wengine ambao wamesugua benchi bila kucheza walau dakika moja ni Ibrahim Parapada wa Singida Black Stars, Lameck Kanyonga wa Mashujaa FC, na Shaaban Kimwaga wa KMC.

Wakato huo huo, kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum, anaongoza kuchangia, mabao mengi katika ligi hiyo ambayo itaendelea tena ifikapo Machi Mosi, mwaka huu.

Fei Toto amechangia jumla ya mabao 13 mpaka sasa kwenye timu yake, akifunga manne na kutoa pasi za mwisho tisa.

Anafuatiwa na kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Ahoua, ambaye amechangia mabao 12 katika  timu yake, akitoa 'asisti' tano na kufunga mabao saba mpaka sasa.

Clement Mzize, Pacome Zouzoua wote kutoka Yanga, na Elis Rupia wa Singida Black Stars wamechangia mabao tisa kwenye timu zao kila mmoja.

Mzize amefunga mabao sita na 'asisti' tatu, Pacome amepachika mabao matano akiwa na 'asisti' nne, huku Rupia anayeongoza kwenye mfungaji kwenye Ligi Kuu na mabao yake manane, ana 'asisti' moja.