MAKAMU Mkuu wa Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Dk. Philemon Langasi, amewapa angalizo Watanzania kuhusu mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwaka huu, akionya wasithubutu kukimbilia kuwachagua na kuwaweka madarakani viongozi wanaotembeza ‘hongo’ ili wachaguliwe.
Amesema viongozi wanaoingia madarakani kwa njia ya fedha, hawaangalii maslahi ya umma zaidi ya kujinufaisha wao n ahata kuwawajibisha huwa ni kazi ngumu.
Akizungumza jana katika Mtaa wa Uzunguni kwa Wasomali, Parokia ya Semento ya Jimbo la Hai la Dayosisi ya Arusha ya Kanisa la KKAM, Askofu Dk. Langasi, amewataka Watanzania kusimama na kumuomba Mungu kupata ufahamu ni kiongozi yupi anayewafaa kumchagua, kwa sababu wanaujua uwezo wa kila mmoja anayetajwa kuwania kiti cha Urais.
Ameyasema hayo, wakati wa ibada maalum ya kuweka wakfu eneo la ibada, kumbariki Mtheolojia Eneza Kitange kuwa Mchungaji na kubariki wazee wa kanisa hilo.
“Namuomba mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan), ambaye katika kipindi chake ameongoza vizuri sana. Tunamuomba aweke ile mifumo ikae sawa sawa ili haki iweze kutendeka. Ninachoamini bado Watanzania wanampenda kwa kazi nzuri alizofanya na watamchagua,”amesema Askofu Dk. Langasi.
Aidha, Askofu Dk. Langasi ameongeza: “Nina wito pia kwa mwaka huu wa 2025, ambao wote kama tunavyojua nim waka wa uchaguzi katika nchi yetu ya Tanzania. Ni mwaka ambao unagubikwa na matukio mbalimbali, matukio ya ajali zisizo na mfano, matukio ya watu kutekwa, matukio ya uharibifu wa kila aina na hata wengine wakiyapa majina kwamba ni utoaji wa kafara.”
Askofu Dk. Langasi, pia ni Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Arusha ya Kanisa hilo la Kilutheri Afrika Mashariki.
Aidha, Askofu mwingine wa kanisa hilo, Dk. Philemon Mollel (Monaban), wakati wa mahubiri, alikemea viashiria vya uvunjifu wa amani katika uchaguzi mkuu ujao, akisema malalamiko madogo madogo yaliyojitokeza wakatu wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwaka 2024 hayapaswi kujitokeza tena uchaguzi mkuu.
Baada ya Mtheolojia, Eneza Kitange, kubarikiwa kuwa Mchungaji mpya wa KKAM, amesema Watanzania wanahitaji kuishi kwa amani, pamoja na uchaguzi mkuu ujao, wanamsihi Mungu ufanyike uchaguzi huru na wa haki.
“Tufanye uchaguzi bila uvunjifu wa amani, tufanye uchaguzi kwa kumtumainia Mungu, kwa kuwa bila kuwa na amani, taifa la Mungu litaangamia. Hatuwezi kuishi maisha ya kumpendeza Mungu kama taifa halina amani,”amesema Mch. Kitange.
Mch. Kitange, amewataka wapiga kura, wasimamizi wa uchaguzi, wapiga debe na watia nia, kuingia kwenye maombi ya kweli, ili taifa liwe na amani kwa wakati huo na baadae.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED