Walimu 201,707 kufanyiwa usaili kujaza nafasi 14,648

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 05:28 AM Jan 12 2025
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.
Picha:Paul Mabeja
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.

WALIMU 201,707 wanatarajiwa kufanyiwa usaili kuanzia Januari 14 hadi Februari 24, mwaka huu, kwa ajili ya kujaza nafasi 14,648 zilizotangazwa na serikali ili kupunguza uhaba wa watumishi wa kada hiyo nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu usaili huo.

“Kuanzia tarehe 14 Januari hadi tarehe 24 Februari, 2025, usaili wa kada za ualimu utaendeshwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (UTUMISHI).

Pia itahusisha Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya, Tume ya Utumishi wa Walimu, Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote na wataalamu mbalimbali kutoka katika Taasisi za Umma, alisema

Simbachawene alisema usaili huo una lengo la kujaza nafasi 14,648, zilizotolewa na Rais kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu nchini.

“Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwasihi sana wale wote walioitwa kwenye usaili wajiandae vyema kwa usaili huo kwani nafasi hizi ni za ushindani.

“Vilevile, kulingana na mahitaji yetu ya elimu kwa sasa, tutaajiri wataalamu wa fani za Amali. Hivyo, nawasihi sana wale wote watakaopata nafasi ya kuajiriwa, wawe tayari kujiendeleza ili kuweza kukidhi matakwa ya ajira zao katika Utumishi wa Umma,” alisisitiza.

Aidha, alisema usaili huo wa kada za ualimu utafanyika katika Mkoa ambao kila msailiwa anaishi lengo ni kuwapunguzia gharama za kusafiri na mambo mengine.

“Sekretarieti ya Ajira ilitoa matangazo kumtaka kila msailiwa kuhuisha taarifa zake katika akaunti yake ya ‘Ajira Portal’ sehemu iliyoandikwa ‘current physical adress’ kwani ndipo tumewapangia vituo vya usaili kulingana na anuani walizojaza,” alisema.

Pia aliwasihi waombaji wote kuhakikisha kila mmoja anakwenda katika kituo ambacho amepangiwa kwa ajili ya usaili kwani mahitaji yake ya msingi yapo huko.

Vile vile, alisema usaili wa awali wa kuandika (Mchujo) kwa kada za ualimu utafanyika kwa njia ya kuandika kwa mkono kwa kada zote na ngazi zote za elimu.

“Ninapenda kuwakumbusha wale wote watakaokwenda kwenye usaili wahakikishe wanabeba vyeti vyao halisi kikiwemo cheti cha taaluma na cheti cha kuzaliwa,”alisema