Momade asajiliwa kuinusuru Prisons

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:34 AM Jan 12 2025
Kocha Mkuu Prisons, Amani Josiah.
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu Prisons, Amani Josiah.

BAADA ya kumsajili straika, Kelvin Sabato 'Kiduku', Prisons imeendelea kukiboresha kikosi chake kuelekea katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, baada ya kupata saini ya kiungo mshambuliaji, raia wa Msumbuji, Amade Momade.

Mkataba huo umesainiwa katika Ofisi za Michezo Makao Makuu ya Magereza jijini, Dodoma na kushuhudiwa na Mkuu wa Kitengo cha Michezo Jeshi la Magereza SSP, Erasto Jackson Ntabahanyi  na Msaidizi wake SSP, Bakari Hamisi Sudi.

Ntabahanyi aliliambia gazeti hili usajili huo umezingatia mahitaji na ushauri uliotolewa na Kocha Mkuu Prisons, Amani Josiah, ambaye amechukua mikoba ya Mbwana Makata, aliyeonyeshewa mlango wa kwaheri hivi karibuni.

Bosi huyo alisema mchezaji hyyo mpya alisaini mkataba wa mkopo na Prisons baada ya kufikia makubaliano na viongozi wake wa Singida Black Stars.

"Tumefanikiwa kumnasa Amade, ambaye atakuwa na sisi hadi mwishoni mwa msimu. Kabla ya kutua kwetu, alikuwa ni mchezaji wa mkopo wa klabu ya Namunngo," ilisema taarifa rasmi iliyotolewa na Prisons.

Taarifa iliwataja wachezaji wengine ambao wamesajiliwa na timu hiyo ni pamoja na   Rabbin Sanga na Athuman Sufian Mwemfua.

Usajili huo ni mkakati maalum kuhakikisha Prisons inafanya vyema katika mzunguko wa lala salama wa Ligi Kuu, baada ya kushindwa kuonyesha makali yake kwenye  mzunguko wa kwanza.

Hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, Prisons iko katika nafasi ya 13 ikiwa na pointi 14 baada ya kucheza michezo 16, ikishinda michezo mitatu, sare tano na imepoteza michezi nane.

Klabu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Kuu ya Wanawake Nchini zinaendelea kujiimarisha huku zikiwa zimebaki siku tatu ili kufungwa na dirisha dogo la usajili.

Ligi hiyo ilisimama kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi, mechi za michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).