KATIKA kuhakikisha inaanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania ikiwa imara, uongozi wa Yanga Princess umetangaza kumsajili aliyekuwa beki wa kati wa Fountain Gate Princess, Protasia Mbunda.
Beki huyo wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), tayari ameshaanza mazoezi na timu yake mpya inayofundishwa na Kocha Mkuu, Edna Lema.
"Ni kweli tumeshakamilisha taratibu za kumnasa Protasia, tunaamini atakuwa msaada mkubwa katika kikosi chetu kuelekea hatua ya lala salama ya ligi, tunataka kujenga kikosi chenye ushindani zaidi," kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kiliongeza tayari kikosi chao kimeshaanza mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mechi za ligi ambayo itarejea tena kuanzia Januari 22, mwaka huu.
Katika msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, Yanga Princess yenye pointi 12 iko kwenye nafasi ya nne nyuma ya vinara, Simba Queens yenye pointi 25 ikifuatiwa na JKT Queens yenye pointi 20 lakini ikicheza mechi moja pungufu.
Mashujaa Queens yenye pointi 15 iko katika nafasi ya tatu wakati Mlandizi Queens ya Mlandizi mkoani, Pwani inaburuza mkia ikiwa na pointi moja.
Ligi hiyo ilisimama kupisha maandalizi ya Timu ya Taifa ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Girls), ambayo ilikuwa inakabiliwa na mechi ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Eswatini, ambayo imejitoa katika michuano hiyo na hivyo Tanzania imesonga mbele.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED