Ripoti Maalum: Utapishaji maji waweka rehani maisha ya watu

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 05:42 AM Jan 12 2025
Chacha Marwa (51), Mkazi wa Mabatini na Mtapishaji wa vyoo jijini Mwanza kupitia kikundi cha Tobazi, akitoa majitaka ndani ya choo akisaidiwa na Samson Makuri.
PICHA: VITUS AUDAX
Chacha Marwa (51), Mkazi wa Mabatini na Mtapishaji wa vyoo jijini Mwanza kupitia kikundi cha Tobazi, akitoa majitaka ndani ya choo akisaidiwa na Samson Makuri.

“SISI wenyewe hatuko salama lakini ndiyo kazi yetu”. Ni sauti ya Samson Makuri, msaidizi wa Chacha Marwa watapisha vyoo kutoka Kata ya Mabatini jijini Mwanza.

Ni katika   mtaa wa Mabatini Kusini, eneo la milimani kando kidogo na Zahanati ya Mabatini, hali ya wakazi wa maeneo haya kwa mwonekano na uchakavu wa majengo inadhihirisha kuwa ni duni.

Majira ya saa 4:00 usiku, watoto kwa wakubwa wanaendelea na shughuli mbalimbali ikiwamo kumalizia mapishi kwa ajili ya mlo wa jioni. Sauti za redio zinazosikika kwa kupokezana katika eneo hili, zinatawaliwa na simulizi tofauti zinazoashiria ni muda wa mapumziko.

Licha ya sauti za redio hizo kulazimu watu wakalale, mwandishi wa ripoti hii anashuhudia watu wawili ambao kwao ndio kumekucha, wakiendelea na kazi ngumu kwa kuitazama lakini ni rahisi na iliyozoeleka kwa mujibu wa maelezo yao. 

Huu ni utapishaji wa vyoo kwa njia za kienyeji wakati wa kiangazi, utaratibu wanaouita kuwa wa kawaida kwa wakazi waishio milimani jijini hapa.

Walichojiandaa nacho wawili hao ambao hali yao ni ya ulevi wakati wote ni mafuta ya taa pekee pamoja na vifaa duni kama vile ndoo, sepetu (koleo) na jembe. Hakuna  glovu wala vifaa maalum vya kujistiri dhidi ya uchafu huo.

Njia hii ambayo si salama, si tu kwao bali hata kwa wananchi wanaoishi maeneo husika, kutokana na hatari ya magonjwa ya mlipuko hususani inaponyesha mvua. Kadhalika ni hali inayosababisha uchafuzi wa mazingira pamoja na hewa chafu wakati wa utapishaji kwa wakazi wa maeneo ya jirani.

Wakati wa kiangazi, wananchi waishio katika baadhi ya maeneo ya milimani, hutumia watapisha vyoo hawa, maarufu kama ‘topazi’ ambao huzibua vyoo na kuhamishia uchafu katika shimo mbadala hali inayoibua pia harufu mbaya katika makazi ya watu. Hali hiyo pia husababisha uchafuzi wa mazingira kwa eneo husika.

SIMULIZI MTAPISHAJI 

Chacha Nyechi (51), Mkazi wa Mabatini Kusini na mtapishaji wa vyoo, anasema alianza kazi hiyo mwaka 1988 na kuwa kazi hiyo amekuwa akiwafanyia wananchi wa maeneo ya milimani hasa wale wenye hali duni na wanaojipatia riziki kwa kufanya shughuli tofauti zisizo rasmi. 

Anasema gharama za kufanya kazi hiyo ni kati ya Sh.70,000 hadi 100,000 kulingana na ukubwa wa choo. Anasema kazi hiyo inahitaji watu wawili hadi watatu kuifanya kutokana na ugumu wake na kuhakikisha wanaifanya kwa ufanisi. 

“Tulitumia hali ya kukosekana kwa miundombinu ya uzoaji wa taka hizi kama fursa baada ya kuona watu wanateseka. Lakini  kazi hii tunaifanya katika mazingira magumu bila kuwa na glovu wala vifaa maalumu vya kufanyia kazi hii, hali inayosababisha tunakuwa hatarini,” anasema. 

Pia anasema wakati wa kufanya kazi hiyo, hujipaka mafuta ya taa kisha mengine humwaga kwenye choo ili kupunguza harufu mbaya wakiwa kazini na kuua wadudu ili waendelee na kazi bila tatizo. 

“Tunaomba serikali itusaidie kupata vifaa ili kufanya kazi hii kwa weledi na kuzikinga afya zetu dhidi ya magonjwa,” anasema Chacha ambaye hata hivyo hali yake ni ya ulevi wakati wote. 

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Mazingira wa Jiji la Mwanza, Desderius Polle, anasema vikundi hivyo vinatambuliwa na serikali na wamekuwa wakipewa mafunzo ya kuhakikisha wanazibua kwenye chemba za watu na kuingiza kwenye mfumo wa maji machafu ili kutokuchafua mazingira na vyanzo vya maji. 

Hata hivyo, hatua hiyo ni tofauti na kinachoendelea mtaani kwa kuwa utapishaji unafanyika katika eneo moja na shimo kuchimbwa pembeni na taka hizo zinafukiwa, hali inayoweza kusababisha mlipuko wa magonjwa pindi mvua ikinyesha.

 Takwimu kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza zinaonesha kuwa zaidi ya  watu 860 katika jiji hilo lenye wakazi takriban 426,154 waliugua magonjwa ya mlipuko yakiwamo kuhara na homa ya matumbo katika kipindi cha miezi sita kuanzia Aprili mpaka Septemba, 2024.

Mlipuko wa kipindupindu uliotokea nchini mwanzoni mwa mwaka 2024, Mwanza iliripoti kifo kimoja na wagonjwa 112 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. 

Kadhalika, ripoti ya Wizara ya Afya ya Mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2023, kipengele cha Majiji na Manispaa iliyotolewa Mei 10, 2024, inaonesha kuwa Mwanza ilishika nafasi ya mwisho kwa kupata asilimia 57 na alama 71 kati 124. Tanga ikiibuka ya kwanza kwa asilimia 84 likifuatiwa na Mbeya 78, Arusha 77, Dar es Salaam 66 na Dodoma 60. Hali hii inaonesha ni kwa namna gani bado kuna haja ya juhudi kuongezwa katika kudhibti uchafuzi wa aina zote.

 HALI WAKATI WA MVUA

Kutokana na jiografia ya jiji la Mwanza, inaelezwa kuwa asilimia 70 ya wakazi wake wanaishi milimani ambako ni vigumu kujenga vyoo vya shimo refu hali inayosababisha kutengenezwa mashimo mafupi na kuachiwa mfumo wa kufungulia uchafu pindi mvua inaponyesha maarufu kama ‘tegesha’.

Bahati Ally (50), Mkazi wa Mtaa wa Nyerere ‘A’, Kata ya Mabatini anasema kwa miaka yote aliyoishi katika eneo hilo wamekuwa wakishuhudia utiririshaji wa kinyesi kutoka kwa wakazi wa maeneo ya juu wakati wa mvua lakini tatizo ni jinsi ya kutambua ni kinanani wanaofanya hivyo.

“Kwa milimani unakuta mtu anapata sehemu ya kujenga choo lakini hana pa kuweka shimo  hali inayosababisha mara nyingi wanategeshea kipindi cha mvua na kumwaga kinyesi.

“Madhara tunayokutana nayo mara nyingi ni pamoja na maradhi hasa kwa watoto, kipindupindu cha mara kwa mara maambukizi kwa njia ya mkojo (UTI) na uchafuzi wa mazingira,” anasema Bahati.

Sehemu ya madhara anayoyataja Bahati, yanathibitishwa kwenye maelezo ya Ofisa Afya wa Jiji la Mwanza, Audiphace Sabbo, anayeitaja kata hiyo kuwa miongoni mwa maeneo kata korofi kwa magonjwa ya kuhara akidhihirisha kuwa hali hiyo inaonesha wananchi wanakula kinyesi.

Anasema kuna haja serikali kutazama suala hilo upya na kuja na mikakati bora ya kutokomeza uchafuzi huo ili kuwalinda wananchi dhidi ya maradhi ya mlipuko hasa katika kipindi cha mvua.

JAMBO LA KAWAIDA

Mkazi wa Sahara Juu, Kata ya Pamba, Juma Abdallah anasema utaratibu huo umekuwa wa muda mrefu kwani wamekuwa wakikutana na vinyesi katika mazingira kutokana na watu kufungua chemba za vyoo na kutiririsha uchafu.

“Mvua ikifululiza lazima ushuhudie hiyo hali na mara nyingi nadhani chanzo ni kwamba wanakwepa gharama za kutapisha vyoo vyao. Ni  vyema serikali iingilie kati hili suala kwa kuboresha miundombinu ili magari yafike juu hasa milimani,” anasema   Abdallah. 

Aidha anasema adha ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo ni pamoja na magonjwa, harufu mbaya kwenye makazi ya watu pamoja na uchafuzi wa mazingira huku akitaka elimu itolewe juu ya athari za utiririshaji vinyesi katika mazingira.

SERA YA MAZINGIRA

Sera ya Taifa ya Mazingira ya 2021 Sura ya Kwanza kifungu cha Pili kifungu kidogo cha 6(1) kuhusu Usimamizi Duni wa Taka za Manispaa, inazitaja taka za maji kuwa tishio kwa mazingira na afya ya binadamu kutokana na kuwa vituo vingi vya mijini nchini havina vifaa vya usimamizi wa taka za maji.

Inafafanua kuwa kati ya Mamlaka 20 za huduma za maji mijini, 11 hutoa ufikiaji wa miunganisho ya mifereji ya majitaka na vifaa vya kutibu maji machafu. ikijumuisha takriban asilimia 13 ya wakazi wa mijini. 

Polle anakiri kuwapo kwa baadhi ya wananchi ambao hawajaunganishwa katika mifumo na kuwa taratibu zinaendelea kufanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), kuhakikisha wanafikiwa na huduma kadiri bajeti inavyoruhusu. 

Anasema wale ambao hawajaunganishwa wanatumia fursa ya mvua inaponyesha kufungulia vyoo vyao ili kuruhusu kinyesi kutiririshwa katika makazi ya watu pamoja na vyanzo vya maji likiwamo Ziwa Victoria.

Polle anasema wamekuwa wakitumia maofisa Afya wa ngazi za Halmashauri na Kata kutoa elimu kwa wananchi na kuhakikisha wanadhibiti utiririshaji maji taka hayo.

“Wananchi kwa kufanya hivyo wanakiuka kanuni na taratibu zetu na kawaida tunasema usafi ni tabia na uchafu ni aibu. Tunaendelea  kuwapa elimu na kuwakumbusha kuwa kufanya hivyo wanaweza kupata adhabu kupitia sheria ndogo zilizowekwa na Halmashauri, anasema Polle.

ATHARI KUBWA 

Kwa mujibu taarifa ya Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Uhifadhi wa Mazingira kwa kipindi cha miaka 10 (2022-2032) kifungu namba 11 kifungu kidogo namba sita kuhusu Athari za Usimamizi Duni wa Taka, Tanzania inakadiriwa kuwa usafi duni unagharimu Sh. bilioni 301 kila mwaka sawa na Dola za Marekani milioni 206. 

Hiyo ni sawa na asilimia moja ya pato la ndani la Taifa (GDP) la Tanzania na Dola za Marekani tano kwa mtu. Hasara za kiuchumi zinahusiana moja kwa moja na kupoteza muda kwa watu wanaotafuta mahali pa kujisaidia, vifo vya mapema, kupoteza uzalishaji wakati wa ugonjwa na fedha zinazotumika kwa huduma za afya.

Kadhalika, Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema takriban asilimia tisa ya vifo vyote vya watoto chini ya miaka mitano na asilimia sita ya vifo katika idadi ya watu wazima, vinahusishwa na kuhara hali inayotokana na ukosefu wa miundombinu ya vyoo.

Ofisa Afya wa Jiji la Mwanza, Audiphace Sabbo, anasema katika kipindi cha robo ya Aprili hadi Juni, 2024 wagonjwa wa kuhara walikuwa 407 huku homa ya matumbo  wakiwa wanane. Anasema Julai hadi Septemba, 2024 wagonjwa wa kuhara walikuwa 408 sawa na ongezeko la mtu mmoja huku homa za matumbo wakiwa 42 sawa na ongezeko la wagonjwa 34.

“Hii ni ishara ya kuwa watu wanakula uchafu maana Typhoid (homa za matumbo)  ni uchafu, hivyo bado kuna tatizo na tunapopata hizi taarifa tunafuatilia kujua ni wapi wanatokea hivyo kwenda na kuchukua hatua,” anasema Sabbo.

Aidha anataja maeneo korofi kwa uchafu na magonjwa ya mlipuko kuwa ni pamoja na Mabatini Kusini, Sinai, Majengo Mapya zote za Kata ya Mabatini, huku Kata ya Isamilo ikiwa na Mitaa ya Isamilo, Nyakabungo, Kaskazini ‘A’, Maendeleo na Msikitini, Kata ya Igogo ni Malulu, Kwimba, Jiwe la Maji na Bugando ‘B’.

Kadhalika, Kata ya Luchelele iliyoko katika mwambao wa Ziwa Victoria, anataja Mitaa ya Silivin, Sweya na Kisoko huku Kata ya Mahina ni mitaa ya Mahina Kati na Igelegele. Kata ya Mkoloni ni Kasese, Nyamazobe na Utemini huku Kata ya Pamba ni Mitaa ya Mission, Bugarika ‘C’ na Mlimani.

“Hizi takwimu zinatokana na maeneo ambako wagonjwa wengi wa kipindupindu walitokea kwenye wimbi la mwaka jana, hivyo wagonjwa wengi walitokea kwenye hii mitaa na kuonekana ni michafu na kama Jiji tukajitahidi kuweka usimamizi ili isijirudie,”anasema.

Pia anasema kutokana na muingiliano mkubwa uliopo kwa Jiji la Mwanza suala la udhibiti na kutoa elimu ni endelevu kwani kila siku wanaingia watu wapya na wenye tabia tofauti.

UCHAFUZI ZIWA VICTORIA

Licha ya utiririshaji huo kutajwa zaidi kusababisha magonjwa, harufu mbaya pamoja na uchafuzi wa mazingira, hali hiyo inatajwa kuwa chanzo kikuu cha uchafuzi wa Ziwa Victoria, hivyo kuwapo hatari ya uhai wa viumbe hai waishio majini pamoja na watumiaji.

Utafiti uliofanywa katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza na InfoNile kwa msaada wa JRS Biodiversity Foundation Machi, 2023 kupitia Mto Mirongo unaoingiza maji ziwani, ulibaini kuwapo kwa kiwango kikubwa cha kemikali ya E.Coli na Coliforms.

 Utafiti huo uliitaja kemikali hiyo kusababishwa na wingi wa kinyesi katika mto huo unaoingiza maji ndani ya ziwa huku ikionesha kwamba maji yalikuwa yamechafuliwa na uwapo wa bakteria watokanao na kinyesi ambao wanaweza kusababisha magonjwa ya majini.

 Ofisa Mahusiano kwa Umma wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), Mhandisi Gerald  Itimbula, anasema kwa sasa hakuna kiwanda chochote wala taasisi inayotiririsha majitaka ambayo hayajatibiwa katika Ziwa Victoria kutokana na takwa la kuweka mfumo wa kutibu maji hayo na kupimwa na maabara ya  LVBWB kuhakikisha usalama wake ndani ya Ziwa.

 “Kilichobaki kwa sasa ni wale wananchi wanaotiririsha majitaka hususani katika kipindi cha mvua. Ziko hatua za utekelezaji wa mradi mkubwa kupitia MWAUWASA utakaodhibiti kwa kiasi kikubwa kero hiyo,” anasema.

MAGONJWA SUGU 

Mkemia na Meneja wa Maabara ya Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria, Frank Baregu, wenye dhamana ya kujua hali ya maji, usalama wake na watumiaji katika eneo lote la bonde la Ziwa Victoria, anasema yako madhara ya muda mrefu na ya muda mfupi yatokonayo uchafuzi wa maji.

Anasema maji hayo yakitumiwa bila kutibiwa yanaweza kusababisha maradhi yakiwamo saratani, figo, misuli, tatizo la fahamu, ngozi kuungua akitolea mfano  kwa tukio lililowakuta wakazi wa Mara pamoja na magonjwa ya kuhara.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano kwa Umma MWAUWASA, Vivian Temu, anakiri kuwapo kwa utiririshaji majitaka katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza. Anasema hali hiyo iko katika maeneo ambayo hayajafikiwa na miradi ya mfumo wa moja kwa moja wa majitaka.

“Baada ya kubaini hali ya uchafuzi, Mamlaka tulikuja na mfumo rahisi ‘simplified sewerage system’ kwa kuunganisha vyoo vyao kwenye mifumo yetu ya majitaka na kupeleka moja kwa moja kwenye mabwawa yetu ya kutibia majitaka katika eneo la Butuja,” anasema Temu.

Pia anasema mfumo huo bado uko kwa maeneo machache yakiwamo Kilimahewa, Pasiansi, sehemu ya Mabatini, baadhi ya maeneo ya Igogo, Kabuholo, Ibungiro pamoja na Isamilo.

Anasema kutokana na gharama za kutengeneza mifumo hiyo kuwa kubwa sana mpaka sasa watu waliofikiwa bado siyo wengi kulinganisha na uhitaji ulivyo mkubwa. 

“Wale ambao hawana mifumo hii wanatengeneza vyoo rahisi na vifupi kutokana na maeneo yao kuwa ya milimani na kuwa na mawe, hivyo wakati wa mvua wanafungulia yale majitaka yanaenda kwenye mito pamoja na Ziwa Victoria,” anasema Temu.

Itaendelea