TAKUKURU yaokoa Sh.milioni 31.4 za viuatilifu

By Baraka Jamali , Nipashe
Published at 06:31 PM Nov 11 2024
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Jumbe Makoba.
Picha: Baraka Jamali
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Jumbe Makoba.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mtwara imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni 31.4 zilizokuwa zimeelekezwa kwenye matumizi yasiyo halali ya viuatilifu kwa wakulima wa zao la korosho kwa msimu wa 2024/2025.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha rasilimali zinawafikia walengwa stahiki bila kuathiriwa na rushwa au ubadhirifu.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Jumbe Makoba, alisema kuwa TAKUKURU kupitia kampeni ya TAKUKURU Rafiki ilibaini changamoto kadhaa kwa wakulima wa korosho katika kijiji cha Chinyanyira, Wilaya ya Nanyumbu. 

Waligundua baadhi ya wakulima walipunjwa viuatilifu vya sulphur, huku wengine ambao hawana mashamba ya mikorosho wakipatiwa viuatilifu hivyo kinyume na utaratibu.

Makoba alieleza, “Uchunguzi wetu ulibaini mifuko 604 ya viuatilifu vyenye thamani ya shilingi milioni 31,408,000 ilikuwa imepangwa kugawiwa kwa watu wasiokuwa na mashamba ya mikorosho. TAKUKURU ilifanya juhudi kuhakikisha viuatilifu hivyo vimegawiwa kwa wakulima halali waliokuwa wamenyimwa.”

Operesheni hii ni sehemu ya malengo ya kampeni ya TAKUKURU Rafiki inayolenga kukabiliana na rushwa kwa kushirikiana na jamii.Makoba alitoa wito kwa wakulima na wananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa kuhusu vitendo vya rushwa ili kusaidia maendeleo ya kijamii.

Aidha, TAKUKURU ilieendelea kutoa elimu ya kuzuia rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024. Bw. Makoba alisema kampeni hiyo inalenga kuhamasisha wananchi kuepuka vitendo vya rushwa na kutoa taarifa iwapo kuna viashiria vya rushwa wakati wa uchaguzi.

“Tunatoa wito kwa wananchi kujiepusha na rushwa wakati wa uchaguzi na kutoa taarifa katika ofisi za TAKUKURU iwapo wataona viashiria vya vitendo hivyo,” alisema Makoba. 

Pia aliwahimiza watoa huduma na wasimamizi wa miradi ya maendeleo kufuata maadili na kanuni ili kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa manufaa ya wananchi.

Takwimu za TAKUKURU zinaonesha kuwa rushwa katika sekta ya kilimo inawakwamisha wakulima na kusababisha hasara kubwa kwa taifa. 

Kutokana na changamoto hizi, TAKUKURU imejizatiti kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwa njia za uchunguzi, elimu, na hatua za kisheria kwa wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Makoba alihitimisha kwa kusema kuwa TAKUKURU imejipanga kuhakikisha inasimamia kwa ukamilifu rasilimali za umma, hususani wakati huu ambapo taifa linaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 

Alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kuimarisha uwazi na haki katika uchaguzi kwa kuepuka rushwa.

Kampeni ya TAKUKURU Rafiki ina lengo la kuwa karibu na jamii kwa kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi. Kampeni hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha matumizi sahihi ya rasilimali, hasa katika sekta ya kilimo ambayo ni mhimili wa uchumi wa taifa.

Viongozi wa jamii wanahimizwa kushirikiana na TAKUKURU ili kuhakikisha vita dhidi ya rushwa vinakuwa endelevu na vyenye manufaa kwa maendeleo ya jamii.