SHIRIKA la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) limeibuka mshindi wa kwanza katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba).
Kutokana na ushindi huo, uongozi wa shirika hilo umetumia fursa hiyo kualika wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwao.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kanali Stanslaus Mishako, aliyemwakilisha Mkuu wa JKT na Ofisa Mtendaji Mkuu wa SUMAJKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, alikaribisha wawekezaji baada ya kutangazwa mshindi katika maonesho hayo yaliyofungwa juzi na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
"JKT jukumu lake ni malezi ya vijana, uzalishaji mali na ulinzi. Kwanini tumekuwa wa kwanza? Ni kwamba jukumu kubwa tulilonalo JKT ni malezi ya vijana ambayo yanakwenda sambamba na kuwafundisha mambo mbalimbali ambayo wakimaliza mafunzo wanajiajiri wenyewe.
"Mahali ambako unaweza kujiajiri kirahisi ni sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kilimo ni uti wa mgongo, hata ukisikiliza mkazo wa serikali ni kuhamasisha vijana kujikusanya katika makundi ili wajiajiri katika kilimo," alisema.
Kanali Mishako alisema kupitia maonesho hayo, JKT imetoa elimu kwa jamii katika sekta hizo zilizowapa ushindi na ndicho pia hufanyika kambini.
"Tunaposema wekeza katika kesho iliyo bora, tunazingatia wananchi na vijana kupata elimu ambayo inahusiana na kilimo, uvuvi na mifugo.
"Ndio maana majaji walipokaa, waliona hilo kwa kuwa maonesho haya ni eneo la kuelimisha umma. Majaji wameridhia kwamba wataalamu tulionao ni wenye weledi wa kutoa elimu.
"Ushirikiano uliopo JKT, umahiri wa wataalamu wa sekta mbalimbali, zikiwamo ujenzi na biashara ni uthibitisho tosha kwa ushindi huu," alisema.
Alisema JKT wakifanikiwa katika nyanja ya chakula kwa kujitosheleza, wataondoa tatizo la uhaba na kuwa na uhakika wa chakula.
Alisema kama kaulimbiu inavyosema, "Tanzania ni Mahali Sahihi kwa Biashara", hivyo rai yao kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi waendelee kuwekeza kwao.
Mkurugenzi wa Huduma na Biashara, Luteni Kanali Dorah Kawawa, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji SUMAJKT, Kanali Petro Ngata, akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu, alisema wao kama Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Kujenga Taifa, wanaitekeleza kaulimbiu hiyo kwa kufanya biashara na uwekezaji.
Alisema kuwa na mashamba, mbuzi, ng'ombe, kondoo, kuku na kujishughulisha na ufugaji nyuki kumechangia kuwapa ushindi katika maonesho hayo.
Vilevile, alisema wanatekeleza majukumu yao katika sekta ya uzalishaji maji ya kunywa, viwanda vya ushonaji nguo na cha utengenezi bidhaa za ngozi na kingine wameingia ubia na China kinachozalisha taa zinazotumia mwanga wa jua.
Pia alisema wana sekta muhimu za huduma na biashara ambapo wanatoa huduma ya walinzi kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu, na sasa wanaweza kuvuka mipaka kwa kuwa wamejitosheleza kwa kupata vyeti vya kimataifa kwa ajili ya kufanya biashara.
Kanali Mishako alisema wanafanya ukandarasi wa kujenga barabara na madaraja, wakiikita pia kuzalisha bidhaa bora katika kampuni kwa kuzingatia uhitaji wa soko na muda.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho hayo katika banda la JKT, Meja Josephat Yongo, alisema, "Banda hili limetuwezesha kupata ushindi mkubwa kutokana na namna tunavyotekeleza sera za kilimo, uvuvi na ufugaji mkubwa. Sisi ni shamba darasa, tunafundisha namna ya kupata mazao katika eneo dogo.
"Hata ufugaji samaki tumefundisha waliotembelea banda letu kwamba unaweza kuwa na eneo dogo ukafuga kwa kufuata masharti unayopewa na wataalamu wetu," alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED