Wanaume wajitosa kutetea haki za wanawake

By Restuta James , Nipashe
Published at 07:49 PM Nov 12 2024
Wanaume wajitosa kutetea haki za wanawake.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wanaume wajitosa kutetea haki za wanawake.

WATETEZI wa haki za wanawake wamewaleta pamoja vijana wa kike na wa kiume, kushiriki katika kubomoa mifumo kandamizi, ikiwamo ndoa za utotoni, ili kuwa na jamii yenye kuheshimu haki za binadamu.

Wakizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Mtandao wa Wanaharakati wa Kifeminia -The Feminist Professional Community Network in Tanzania, wamesema mifumo kandamizi dhidi ya wanawake na watoto, inahitaji juhudi za pamoja.

Mwanaharakati Lazaro Saranga (Loso), amesema wanaoendeleza ndoa za utotoni ni wanaume na kwamba wao wana nafasi ya pekee kuzipinga.

“Tumefundishwa maarifa yanayotuwezesha kuelimisha jamii hasa katika kutetea usalama wa watoto na wanawake, ambao ni waathirika wakubwa wa unyanyasaji wa kijinsia. Wanabakwa, wanalawitiwa na wanapigwa. Sisi wanaume ndio watendaji wa ukatili huu,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Sisi wanaume ndio kaka, baba, wajomba na walinzi wa familia, tukishiriki kupinga, matokeo yataonekana haraka zaidi kuliko tukiwaachia wanawake peke yao.” 

Amesema sauti za wanaume katika kupigania haki za kijamii ni muhimu kwa kuwa zinasaidia kuandaa kizazi cha wanaume wanaojua wajibu wao.

“Sisi wanaume ndio tunaobaka, tunalawiti na tunaoa watoto wadogo. Kwa kuwa sisi ndio wahusika wakuu wa matendo haya, tumekuja msitari wa mbele kuwaelimisha wanaume wenzetu tuache tabia hizi. Tuache tabia hizi mbaya,” amesema.

Anneth Mirambo, ametoa rai kwa wanawake na mabinti kuchangamkia fursa zinapotea hususani uandishi wa vitabu, vya kuelimisha jamii kuhusu mambo yanayoizunguka.

 Kwa upande wake, mshauri wa wanaharakati hao, Getrude Malizeni, amesema kwenye sanaa kuna fursa nyingi za wanawake ambazo wakizitumia wanaweza kujiingizia kipato na pia kuelimisha jamii.

Meneja wa Mawasiliano wa mtandao wa watetezi hao, Catherine Madebe, amesema lengo la kuibua wanaharakati wapya ni kuongeza wigo wa kupinga unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike.

Amesema wameandaa washauri watakaowasimamia wanaharakati chipukizi, ambao watasaidia kupinga unyanyasaji.