PSSSF yawapa mbinu wastaafu watarajiwa jinsi ya kuishi nje ya utumishi wa umma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:10 PM Nov 12 2024
PSSSF yawapa mbinu wastaafu  watarajiwa jinsi ya kuishi nje  ya utumishi wa umma
Picha: Mpigapicha Wetu
PSSSF yawapa mbinu wastaafu watarajiwa jinsi ya kuishi nje ya utumishi wa umma

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekutana na wanachama wake wa Mkoa wa Mbeya wanaotarajia kustaafu hivi karibuni na kuwapa mafunzo (mbinu) bora ya kuishi baada ya kustaafu utumishi wa umma.

Akiwapa mbinu hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Meneja wa Pensheni za Wastaafu, Kwame Temu, amewaambia kuwa ni busara mara mstaafu atakapopokea Mafao yake, awekeze katika viwanda vidogo vidogo na vya kati, uwekezaji katika masoko ya fedha, kilimo biashara na ujasiriamali kwa ujumla.

“Mafao ya uzeeni yanayolipwa kwa wastaafu yakitumika vizuri yanaweza kutoa mchango katika kuendeleza miradi mbalimbali, kutengeneza ajira kwa vijana, kuongeza pato la mstaafu na hatimaye pato la Taifa.” amesema Temu.

Aidha mgeni rasmi katika mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya mjini, Benno Malisa, yeye amewaasa kuzingatia mafunzo hayo.

“"Kati ya zawadi ambayo PSSSF imewapa wastaafu ni mafunzo haya, tuwashukuru sana, tutumie fursa hii kusikiliza kwa makini mafunzo mnayopewa na PSSSF pamoja na elimu inayotolewa na wadau wa sekta za fedha ili fedha zenu muwekeze sehemu sahihi na salama msije kumbana na matapeli.” aliasa

Aidha amewaonya kujihadhari na washaru watakaoibuka katika kipindi hiki ambacho wanajua kuwa wastaafu watapokea malipo.
“Watu wanajua sasahivi kuna pesa mtapata hivyo washauri watakua wengi, mjiepushe nao," alionya.