BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imekiri kuwapo kasoro kwenye shughuli za ukopeshaji mitandaoni, ikirejea kati ya maombi 16 iliyopokea, manne pekee ndiyo yamekidhi vigezo. Sambamba na hilo, BoT imebaini ukiukwaji wa sheria kwa Watoa Huduma Ndogo za Fedha (Microfinances) kuanzisha ‘aplikesheni’ za kukopesha mtandaoni kinyume cha sheria walizowekewa.
Ni ufafanuzi uliotolewa na Meneja Msaidizi Idara ya Microfinance wa BoT, Mary Ngasa, alipozungumza na Nipashe ofisini kwake wiki iliyopita jijini Dar es Salaam kuhusu kuwapo ukiukwaji huo wa sheria, hata kudhalilisha wakopaji. “Kati ya maombi ya aplikesheni 16 kwa ajili ya kutoa mikopo mtandaoni, manne pekee yamekidhi vigezo na kupewa leseni za kukopesha mtandaoni, huku aplikesheni 55 zilikabidhiwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili waziondoe mtandaoni,” alisema.
Mary alisema aplikesheni zilizopewa kibali, zinatakiwa kuweka wazi kuwa zinafanya kazi kwa mujibu wa leseni inayotolewa na BoT, kuweka wazi masharti ya mikopo na mawasiliano ambayo wateja wanaweza kuyatumia kuwasiliana nao kwa jambo lolote.
Alisema BoT pia imebaini aplikesheni hizo zina muunganiko na Microfinances ambazo zimetumia fursa ya kuwapo tekonolojia, kuanzisha aplikesheni za kukopesha mtandaoni, na kwamba zipo microfinances zenye hadi aplikesheni 10 za kukopesha mtandaoni.
“BoT imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya Microfinances nne ambazo zilianzisha aplikesheni na kutoa mikopo mtandaoni bila kibali cha BoT kama leseni yao inavyowataka. “Wanaotoa mikopo mtandaoni bila kibali, waliogundulika hadi sasa ni 55 na licha ya tangazo kuwataka wajisajili hawajafanya hivyo.
Tulivyotoa mwongozo wa kuwataka walete maombi hawajaleta, lakini tumewafuatilia mtandaoni na kuwabaini,” alisema. Akifafanua zaidi, Ofisa Idara ya Microfinance, Deogratius Mnyamani alisema: “Tulianza uchunguzi wetu muda mrefu, tukabaini kuna zaidi ya aplikesheni 71, tukaona taratibu zao, baadhi tuliwaita tukazungumza nao, ndipo tukatoa mwongozo, huwezi kuutoa hewani, lazima uwe umejiridhisha na mambo mengi.
“Leseni ya Microfinance inaruhusu kuongeza bidhaa nyingine, lakini wengi wakati wanaomba hawakueleza kwamba watakuwa wanatoa mikopo mtandaoni, na tulipofuatilia zaidi, tukabaini kuna wenye Microfinance moja lakini wana aplikesheni 10.
“BoT tunaposimamia tunataka kufahamu taarifa za utendaji wake wa kila mara, lazima atuletee sera ya ukopeshaji ambayo tunaipitia ili kujua aina ya mikopo, kiwango cha mikopo, muda, riba, namna ya ufuatiliaji, urejeshaji na dhamana. Anapotaka kufanya mabadiliko yoyote lazima atuletee BoT ili tuone kama inafikia viwango na masharti yaliyowekwa.”
Kaimu Meneja wa Microfinance, Dickson Gama alisema BoT ilijipa muda kuchunguza suala hilo na kupata uzoefu wa nchi zilizopitia changamoto kama hiyo ili kuwa na mwongozo, na kwamba usimamizi wa huduma ndogo za fedha uliletwa kwenye benki hiyo mwaka 2018. “Tulikuwa na watoa huduma binafsi wengi, vilio vilikuwa vingi kwa watu kutapeliwa mali, ndipo uhitaji wa sheria ya kusimamia hii sekta uliibuka,” alisema.
Kuhusu udhalilishaji wakopaji mtandaoni unaoshuhudiwa nchini hivi sasa, Gama alisema: “Utaratibu ni kwamba mtu amekopa, hajalipa unampa notisi ya siku 14, hajajibu anapewa ya siku saba na baada ya hapo unachukua hatua kwa utaratibu kwa kuchukua dhamana yake kwa njia ya kisheria, lakini wanapotishia watu, wanavunja sheria nyingine za nchi.”
Alisema ufuatiliaji wa BoT utakuwa endelevu. Kila mtoa huduma atachunguzwa na akibainika kuvunja sheria, watamchukulia hatua kwa kushirikiana na TCRA.
“Kama nchi nadhani itafika wakati tutawatafuta hata ‘Play Store’ ili wasizipandishe hadi wapate kibali cha mamlaka. Kuna nchi Google hapandishi aplikesheni zake hadi ajiridhishe na mambo ya kisheria,” alisema. Alifafanua kuwa hivi sasa kila mwenye aplikesheni aliyesajiliwa na BoT, lazima aoneshe ni nani, kibali alichopewa, namba ya leseni ya BoT na mawasiliano, na kwamba siku zijazo wataboresha ili kuwa na namba maalumu ya utambuzi kama imesajiliwa au la.
“Mikopo ya mtandaoni imetokea kutokana na maendeleo ya teknolojia ili kuwezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi kokote aliko.
Hata hivyo, kuna changamoto watu wanatukanwa na kudhalilishwa, ila tumechukua hatua madhubuti kudhibiti kwa sababu ni jukumu letu kuhakikisha sekta iko salama,” alisema. Ofisa huyo wa BoT alisema Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018, inaelekeza taasisi kuwa na wafanyakazi au chombo cha kupokea malalamiko kutoka kwa wateja ili kunapokuwa na changamoto, wawe na mahali pa kutolea dukuduku na ikishindikana ndipo wanaweza kwenda BoT.
“BoT tunasajili taasisi, ikishasajiliwa inaruhusiwa kutoa huduma, walaji wakiona wametendwa kinyume kama vile udhalilishaji, kutukanwa, kunyanyaswa, kusambaza taarifa kwa mtu mwingine, wana haki ya kumshtaki kwa mujibu wa Sheria ya Taarifa Binafsi (2022).
Ili huyu mkopeshaji atoe huduma, ni lazima ajisajili kwenye Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania (PDPC). “BoT tumeona katika ufuatiliaji wetu, kuna watu walikwenda polisi wakashtaki na kupata haki kama inavyostahili kwa mtanzania yeyote ambaye atatukanwa au kusambaziwa taarifa zake kwa watu wengine kinyume cha ridhaa yake, ana haki ya kuwashtaki,” alisema.
Meneja Msaidizi Idara ya Microfinance wa BoT, Mary Ngasa alisema kuwa baada ya mwongozo wa mikopo mtandaoni, walitoa taarifa ya namna ya kusajili na tangazo kwa umma liliwataka wakopeshaji wawasilishe maombi ili yapitiwe na kupewa kibali. “Tulitoa muda wa siku 14 walete maombi, wapo walioleta tumeyachakata na wamepewa vibali.
Tulitaka kufahamu wanaofanya hizo biashara, ambaye ataendelea bila kibali tutachukua hatua kwa kushirikiana na TCRA, kuwatoa kwenye mtandao,” alisema. Oktoba 21, 2024, Nipashe ilichapisha ripoti ikiangazia namna ukopeshaji mtandaoni ulivyogeuka kero, ikiwamo udhalilishaji wananchi.
Uchunguzi wa Nipashe pia ulibaini masharti ya mikopo hiyo yanafichwa, riba kubwa inayozidi asilimia 80, huku Mbunge wa Viti Maalumu akieleza kwamba, wanawake 68 katika mikoa minane nchi wamefariki dunia kutokana na udhalilishaji baada ya kukopa.
Kazi hii imefanikishwa kwa msaada wa German Federal Foreign Office kupitia Deutsche Welle (DW).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED