Mwenyekiti wa Bunge la Bonanza na Mbunge wa Jimbo la Makete, Festo Sanga, ametangaza kuwa Bunge limeandaa bonanza litakalojumuisha mashabiki wa timu za Simba na Yanga, likitarajiwa kufanyika Januari 25, 2025, katika Viwanja vya John Melin, Miyuji, Dodoma. Bonanza hilo litashirikisha michezo mbalimbali kwa timu hizo mbili.
Akizungumza jana katika Ofisi Ndogo za Bunge, Posta, Dar es Salaam, Sanga ameeleza kuwa lengo la bonanza hilo ni kuhamasisha michezo nchini na kuchangia juhudi za kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kama presha na kisukari.
Azania Bank itadhamini bonanza hilo, na benki hiyo imeahidi kuhakikisha litafanyika bila changamoto, kwa ushirikiano na serikali.
"Tumeandaa bonanza hili kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Bunge na taasisi mbalimbali, na pia kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha michezo nchini," amesema Sanga.
Rais wa TFF, Wallace Karia, amelipongeza Bunge kwa mpango huo, akisema ni njia nzuri ya kuheshimu timu hizo mbili kubwa nchini na kupunguza athari za magonjwa yasiyoambukiza.
Aidha amesema timu hizo mbili zimekubali kuishiriki katika bonanza hilo, ili kudumisha umoja katika michezo baina ya timu hizo na kuwa bonanza hilo liwe na mwendelezo wa michezo mbalimbali ambayo inapendwa na kundi la watu wengi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Azania Bank, Agustino Matutu, amesema benki hiyo inaandaa bonanza la mwaka huu kuwa bora zaidi kuliko lililopita na kuwa washiriki wa bonanza hilo kwa dhati ili kuhamasisha Watanzania katika michezo.
“Tunajivunia kuwa tumekuwa wadhamini wa bonanza hili, kuwa ni sifa na tunaona fahari kushiriki kwahiyo tunawakaribisha watanzania kushiri bonanza hili na pia tunajenga umoja wa taifa katika michezo kwasababu tunawaleta watanzania wote kwa pamoja,” Matutu amesema
Uongozi wa timu za Simba na Yanga pia umepongeza Bunge kwa kuandaa bonanza hilo, na kutoa wito kwa mashabiki wa timu hizo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hilo la kitaifa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED