SMZ yajipanga kusitisha uvuvi haramu Chwaka

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:30 AM Jul 27 2024
WAZIRI wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman
Picha: Mtandao
WAZIRI wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman

WAZIRI wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman, amesema wizara yake inaendelea kutafuta ufumbuzi wa kusitisha uvuvi haramu katika ghuba ya Chwaka wanaotumia nyavu ndogo.

Aliyasema hayo ofisini kwake jana Mjini Zanzibar, wakati akizungumza na viongozi wa wizara hiyo, kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Kusini Unguja, wananchi na  wavuvi wa ukanda wa ghuba ya Chwaka kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kuwapatia suluhu.

Waziri  alisema wizara imeamua kutafuta  ufumbuzi wa kutengeneza boti kubwa za uvuvi zenye urefu wa mita nane na uwezo wa kufika kina kirefu cha maji kwa ajili ya ukanda wa kusini hususan ghuba ya Chwaka.

Alisema hatua hiyo itasaidia eneo lililotengwa kwa ajili ya uhifadhi liendelee kuzalisha samaki wengi zaidi pamoja na kutoa nyavu ambazo zinaruhusiwa kutumika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na serikali.

Waziri Shaaban alisema wizara iko tayari kusikiliza maoni ya wavuvi na kuyafanyia kazi ili kuleta tija  kwa pande zote mbili na kuhakikisha suala la uvuvi haramu linaondoka kabisa katika ukanda wa ghuba ya Chwaka.

Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahamoud, alisema kukimbizana na wavuvi na wasimamizi wa eneo la hifadhi la samaki  si jambo zuri  na linahatarisha usalama wao, hivyo ni vyema wavuvi hao kukubaliana na  mapendekezo yaliyotolewa na serikali ili kupata ufumbuzi wa haraka.

Wavuvi wa ghuba ya Chwaka walisema wameyapokea maelekezo yaliyotolewa na serikali sambamba na kuiomba Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu kupitia wataalamu wake kuendelea kufanya uchunguzi wa kina juu ya matumizi ya bahari kwa ukanda wa ghuba ya Chwaka.

Juma Khamis, mmoja wa wavuvi hao, alisema hatua hiyo itafanikisha dhamira ya serikali ikiwamo ya kuondoa changamoto zilizopo sasa kwa wavuvi.