MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amekutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda.
Katika kikao hicho kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa iliyoko, Ilala Boma jijini, Kamishna Mkuu Mwenda aliongozana na baadhi ya wataalamu wa mamlaka hiyo.
Chalamila, pamoja na mambo mengine, alizungumzia mambo kadhaa yaliyojadiliwa ikiwa ni kupunguza migogoro ya kikodi inayolalamikiwa na wafanyabiashara na kutanua wigo wa walipakodi kulingana na vyanzo vingi vya mapato vilivyomo katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa, Chalamila pia alisema wamezungumzia kuboresha miundombinu ya kikodi ili TRA ikusanye mapato zaidi.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu Mwenda alimshukuru Chalamila kwa ushirikiano anaotoa kwa kufanya kazi na TRA katika wilaya zote tano za Dar es Salaam na kuthibitisha kuwa mkoa huo ni kitovu cha biashara kwa kuwa unakusanya kodi zake zote kwa takribani asilimia 80.
Mkuu wa Mkoa Chalamila alipongeza TRA kwa jitihada mbalimbali inazochukua kutanua wigo wa kodi na kuahidi ushirikiano na kuhakikisha kodi inakusanywa kwa maendeleo ya taifa.
Hivi karibuni Mkoa wa Dar es Salaam ulikumbwa na migomo ya wafanyabiashara katika baadhi ya masoko, yakiwamo Soko la Kimataifa Kariakoo na machinga wa eneo la Simu 2000, wilayani Ubungo, mgomo ambao baadaye ulichukua sura ya kitaifa, hata kusababisha kufanywa mabadiliko katika Baraza la Mawaziri.
Mkuu wa Mkoa Chalamila ni miongoni mwa watendaji wa serikali waliojitokeza hatua za awali kutatua mgogoro huo, akizungumza na wafanyabiashara walioitisha migomo Kariakoo na Simu 2000.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED