KATIKA kipindi cha miaka 25 iliyopita, Tanzania imetekeleza dira ya maendeleo ya taifa 2025, ambayo ililenga kuinua uchumi wa nchi hadi hadhi ya kipato cha kati.
Dira hiyo iliyoanza kutumika mwaka 2020 inafikia ukomo na sasa taifa limeanza nyingine ya 2050.
Kupitia dira hiyo, Tanzania ilifanya mengi ikidhamiria kufanya mageuzi makubwa ya kimaendeleo ya kijamii na kiuchumi ambayo yatalingana au kuzidi ya nchi za kipato cha kati ngazi ya juu.
Ili kufikia lengo hilo, rasimu ya dira 2050 inasema Tanzania imedhamiria kuwa nchi yenye hadhi ya kipato cha kati ngazi ya juu, ikichagizwa na sekta ya uzalishaji viwandani.
Lengo ni kufikia pato la mtu la kati ya Dola za Marekani 4,700 sawa na Sh. milioni 11.6 hadi 8,000 karibu Sh. milioni 19.8, huku pato la taifa likifikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 700, ifikapo 2050.
Kuondoa umaskini uliokithiri na kupunguza kiwango cha umaskini wa mahitaji kuwa wa chini ya asilimia tano. Tanzania kuwa nchi kinara katika uzalishaji wa chakula barani Afrika na kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa 10 wa chakula duniani.
Vilevile, shabaha nyingine ni kuwa na mazingira bora ya kufanya biashara na kushika nafasi ya tatu kwa ubora barani Afrika katika kuvutia wawekezaji.
Aidha kuwa na sekta binafsi imara na yenye ujasiri na uwezo wa kiushindani,
kikanda na kimataifa. Pamoja na hayo shabaha nyingine ya dira ni kukifanya Kiswahili kuwa lugha inayoheshimika na kutumika ukanda wa Afrika Mashariki na moja ya lugha rasmi zinazotumika kwenye Jumuiya ya Umoja wa Mataifa.
Kuwa na mfumo bora wa elimu katika ngazi zote unaojenga maarifa na stadi za wahitimu na wenye kushabihiana kwa karibu na sekta za uzalishaji. Aidha, kuwa na jamii yenye afya njema ambapo kila Mtanzania anapata huduma bora za afya, maji na hifadhi ya jamii.
Kuwa taifa linalojitehemea kwenye umeme ambapo wastani wa matumizi ya uememe wa mtu ninafsi yatakuwa angalau kilo wati 600 kwa saa.
Pia shabaha nyingine ya dira 2050 ni kuwa na jamii inayothamini kuhifadhi mazingira na iliyotayari kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Tanzania kuwa kitovu cha huduma za usafirishaji shehena katika ukanda wa Afrika, kuwa na jamii yenye maarifa ya kidijitali na uwezo wa kutumia zana na kuzalisha teknolojia ya kidijitali katika huduma za uzalishaji.
Shabaha nyingine ya dira hii ni kuifanya Tanzania kuwa taifa la kidemokrasia likiongozwa na katiba imara inayoakisi mwafaka wa kitafa, taasisi madhubuti za umma na mfumo thabiti wa vyama vingi vya siasa, shabaha nyingine ni Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa 10 bora duniani na kushika nafasi ya kwanza barani Afrika katika kupunguza pengo la kijinsia kwa asilimia 35 ifikapo mwaka 2050.
Kuongeza wastani wa umri wa kuishi kwa wanaume na wanawake kufikia miaka 75, kadhalika kuwa kinara barani Afrika kwenye vivutia watalii na miongoni mwa nchi bora Afrika zinazotembelewa na watalii kwa wingi.
Kila Mtanzania kuwa na elimu angalau kidato cha nne na angalau asilimia 15 ya Watanzania kuwa na elimu ya juu wakiwa naujuzi stahiki unaolingana na mahitaji ya soko la ajira na dunia inayobadilika, angalau mmoja katika Watanzania wawili mwenye sifa za kuajiriwa katika sekta rasmi na wakiwa na mikataba kamili ya ajira.
Shabaha nyingine ya dira 2050 ni Watanzania wote wafurahie uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kukusanyika katika mazingia ya amani usalama na utulivu.
Wakati shabaha ya mwisho ni ardhi yote ya Tanzania kupangwa na kupimwa kwa matumizi mbalimbali. Kwa ajili ya makazi bora kilimo, mifugo na uwekezaji
MUUNDO/MALENGO
Dira ya 2050 imegawanyika katika maeneo manne ya msingi mkuu ambayo ni utawala, amani, usalama na utulivu.
Eneo hili ndilo jiwe na msingi linalobeba mengine yote kwa hiyo kuyumba eneo hilo kutayumbusha mengine yote.
Nguzo kuu zinazobeba dira ziko tatu nazo ni uchumi imara, jumuishi na shindani, pia kuwa na watu wenye uwezo, maendeleo ya jamii, uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu kwenye mabadiliko ya tabianchi.
Kufikiwa kwa malengo ya dira 2050 kunategemea ufanisi wa utekelezaji wa nguzo hizo.
VICHOCHEO
Haya ni maeneo yanayochochea kasi ya utekelezaji wa maeneo mengine ya dira ili kuleta tija, ufanisi na ubunifu.
Navyo ni pamoja na sekta za kimageuzi ambazo pia huitwa sekta kipaumbele ambazo utekelezaji wake unategemewa kuchagiza na kuwezesha ukuaji wa uchumi kufikia lengo la taifa la kuwa na uchumi wa kati wa ngazi ya juu.
Aidha, lengo la msingi mkuu wa dira hii ni kuwa na mifumo imara ya kisheria na kitaasisi katika kuwezesha utekelezaji endelevu na wenye ufanisi wa dira 2050.
Maeneo yatakayozingatiwa ni utawala bora na haki za jamii. Katika ngazi mbalimbali serikalini na taasisi za mifumo yote ya kijamii itakayohamasishwa na kuwepo na utawala wa sheria, demokrasia, kupinga unyanyasaji wa aina zote, kupiga vita rushwa na kudumisha uhuru wa Asasi za Kiraia (AZAKI).
Aidha, kuwa na serikali imara za mitaa zenye ufanisi ni sehemu ya dira hiyo, zinazojitegemea, zenye ubunifu, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na zinazowajibika na kutoa huduma bora kwa jamii.
Uwajibikaji katika utumishi wa umma, sifa hii inayoongozwa na matamanio ya kuwapo watumishi wa umma wenye maadili, kuzingatia weledi na utawala wa sheria.
Vile vile dira inasisitiza umuhimu wa raia kuzingatia sheria na kupiga vita maovu.
Aidha, amani usalama na utulivu ili kuwepo kwa taifa imara, tulivu lenye umoja licha ya tofauti za dini, kabila na jinsia ni sehemu ya dira hiyo.
Kadhalika kufikia taifa lenye watu wenye uwezo wa kubaini fursa, kutabiri matukio mapema ili kuweka mifumo madhubuti na kujikinga na majanga na kulinda maslahi ya taifa.
Nguzo ya kwanza ya uchumi imara, jumuishi na shindani lengo lake ni kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuimarisha ushindani na uwazi na kuwezesha utabiri wa sera za kiuchumi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kufikia uchumi imara, jumuishi na endelevu.
Maeneo ya kuzingatia ni pamoja na kuwapo sera za fedha, mapato na kodi zenye kutabirika zitakazozingatia uwiano, vigezo muhimu kama mapato na matumizi, urari, akina na uwekezaji, uzalishaji na mahitaji.
Ubunifu katika vyanzo mseto vya mapato. Katika eneo hili matamanio ni kuimarisha ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi pamoja na soko la fedha katika kugharamia shughuli za maendeleo.
Kuwapo na mazingira yenye kuvutia, kulinda, kuendeleza uwekezaji na biashara, yatakayowezesha kuwapo kwa sera endelevu na zinazotabirika pamoja na kupunguza gharama za uwekezaji na biashara.
Aidha, kuanzisha mashirika ya umma ya kimkakati na kuwa na mashirika ya umma madhubuti na yenye ufanisi , viongozi na watendaji waadilifu, kuendeshwa kwa uwazi na uwajibikaji ni shabaha ya dira.
Kadhalika mashirika hayo yafanyekazi kwa uwazi, kuvutia uwekezaji mbalimbali na kuzingatia faida ili kuharakisha maendeleo kiuchumi na utoaji wa huduma za umma ndicho dira inachotazamia.
ITAENDELEA WIKI IJAYO
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED