BAADA ya kuiaga 2024 na kuikaribisha 2025, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kuliendeleza taifa kuanzia kwenye sekta ya elimu ndiyo suala la kipaumbele.
Kwa kuzingatia mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ambayo dunia imeshuhudia, bila shaka Tanzania inatarajia mambo makubwa zaidi katika tasnia ya teknolojia yanayohitaji kusimamia TEHAMA kwenye kufundisha ili kufanikisha kutekeleza dira ya maendeleo ya taifa ya 2050.
Ndiyo maana katika juhudi za kuboresha masomo ya sayansi na teknolojia, serikali inawapa mafunzo maalum walimu wa sayansi, TEHAMA, kupitia mradi wa kuimarisha elimu ya sekondari (SEQUIP).
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, anayeshughulikia Elimu, Dk. Charles Mahera, anatinga Tarime mkoani Mara, kufungua mafunzo ya walimu wa masomo hayo wa mikoa ya Mara na Simiyu.
Lengo la mafunzo ni kuwawezesha walimu kutumia mbinu za kisasa za ufundishaji, kama TEHAMA kuongeza ufanisi na ujuzi wa wanafunzi katika masomo ya sayansi, hisabati na teknolojia, ili kuwaandaa kuwa wataalamu na wavumbuzi wa masuala mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Dk. Mahera anasema hizo ni jitihada za kuhakikisha walimu wanapata mafunzo ya kisasa yanayoboresha mbinu za ufundishaji.
Anasisitiza kuwa mafunzo hayo ni muhimu ili kuboresha ufundishaji sayansi, hisabati na TEHAMA, ili kuwajengea uwezo wa kuandaa na kutumia zana bora za kujifundishia na kujifunzia kutokana na mazingira yao.
Dk.Mahera anafafanua kuwa, hadi sasa walimu zaidi ya 29,000 wameshanufaika na mafunzo hayo, na lengo ni kuwafikia walimu 40,000 ifikapo Januari 2026.
“Mafunzo haya, yanahusisha matumizi ya teknolojia ya kisasa kufundisha, ambayo yatawezesha walimu kuwafundisha wanafunzi kwa njia bora zaidi na kuwaandaa kuwa wataalamu wa sayansi, hisabati na TEHAMA katika siku zijazo,” anasema Dk. Mahera.
Anawasisitiza walimu, kumudu matumizi ya Kiingereza katika kufundisha na kujifunza TEHAMA.
Mratibu wa Mradi wa SEQUIP, Dk. Nicholaus Gati, anasema mradi huo unakusudia kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi wa sekondari na kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.
Anasema malengo ya mradi ni wanafunzi, hususan wa kike, wapate elimu ya sekondari na kumaliza masomo kwa mafanikio.
“Mradi huu ni wa miaka mitano, ulianza Novemba 2021 na utakamilika Januari 2026 kwa kutumia Sh. trilioni 1.2, tutaongeza fursa za elimu kwa wasichana ili wapate elimu ya sekondari kwa usawa na kuimarisha matumizi ya TEHAMA kwenye elimu ya sekondari,” anasema Dk. Gati.
Mkurugenzi wa Ualimu, Huruma Mageni, anasema walimu wamefundishwa kutumia mbinu za kisasa ambazo zinakuza ubunifu, kutumia TEHAMA, ili kuwawezesha wanafunzi kufikia malengo kwa ufanisi na urahisi zaidi.
“Kwa kuzingatia juhudi zinazofanywa katika kuboresha elimu ya sekondari kupitia mbinu shirikishi na mafunzo endelevu kwa walimu, kuna matumaini makubwa ya kuongeza ufanisi katika masomo ya sayansi, hisabati na teknolojia,” anasema Mageni.
Ni muhimu katika kukuza uwezo wa wanafunzi, ili kuwaandaa kuwa wataalamu na wabunifu wenye ujuzi wa masuala mbalimbali, mafunzo hayo, yanaweka msingi wa maendeleo ya kitaaluma na kiuchumi, ambayo yatajenga jamii yenye ufanisi na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kisasa duniani.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, mhadhiri mwandamizi wa fizikia kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (MUCE) cha mkoani Iringa, Dk. Talam Kibona, anasema ni hatua muhimu ya kuleta mabadiliko katika ufundishaji wa sayansi na teknolojia.
Anasisitiza kuwa bila fizikia, si rahisi kupata wataalamu kama wahandisi, madaktari au marubani, na kwamba walimu waliojengewa uwezo wa kufundisha masomo hayo kwa ufanisi watakuwa na mchango mkubwa katika kuwatengeneza wataalamu wa fani hizo kwa mustakabali wa taifa.
Dk. Kibona anaongeza kuwa mabadiliko ya mitaala yanalenga kuendana na mahitaji ya kisasa ya elimu, ambapo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika kutoa elimu bora kwa nchi zinazoendelea.
Mhadhiri mwandamizi, Idara ya Kemia, UDSM, Dk. Grace Kinunda, anaeleza kuwa mafunzo waliyoyatoa yanawawezesha walimu kutumia mbinu mbalimbali shirikishi kwenye ufundishaji na ujifunzaji, kwa vitendo.
Anasisitiza kuwa, kupitia mbinu hizo kemia itakuwa rahisi kueleweka na kupendwa na wanafunzi ukilinganisha na ilivyokuwa awali kabla ya walimu kujengewa uwezo wa kutumia mbinu za kisasa kwa vitendo katika ufundishaji.
“Kwa muda tuliokaa darasani na walimu wameona kuwa mbinu hizi zitamaliza mada kwa ufanisi, hata katika madarasa makubwa, na kuwafanya wanafunzi kushirikiana na kutafakari pamoja kwa kina,” anasema Dk. Grace.
Aidha, katika mafunzo hayo Grace anawasisitizia walimu, umuhimu wa kutumia vifaa vilivyopo katika mazingira yao, badala ya kutegemea vifnavyotoka viwandani wanapofanya majaribio ya kemikali.
Anasema juhudi zitapunguza gharama na kuhamasisha matumizi bora ya rasilimali zilizopo.
Anaonyesha wasiwasi kuhusu ushiriki mdogo wa walimu wanawake katika mafunzo hayo na kusema ni muhimu kuongeza idadi yao ili kuondoa dhana potofu katika jamii kuwa masomo ya sayansi ni ya wanaume pekee.
Anakazia umuhimu wa kuwajumuisha walimu wenye ulemavu katika mafunzo hayo akisema ni muhimu kushiriki kwa wingi ili wajifunze kutumia mbinu mbalimbali za ufundishaji na kuwasaidia wanafunzi wao, bila kujali changamoto yoyote waliyonayo.
Dk. Lilian Mulamula, Mhadhiri wa Idara ya Bailojia UDSM, anaeleza kuwa matumizi ya TEHAMA ni kiungo kufanikisha ufundishaji wa kisasa, kwani inawasaidia walimu kuandaa zana mbalimbali za kufundisha kwa vitendo.
Anasema teknolojia hiyo, inawawezesha wanafunzi kushiriki kikamilifu katika darasa, jambo ambalo linajenga ufanisi na kuelewa somo kwa vitendo.
“Moja ya mabadiliko makubwa yaliyoletwa na mafunzo haya ni matumizi ya teknolojia katika kufundisha na kujifunza, walimu wamejengewa uwezo wa kutumia vifaa vya kisasa kama kompyuta, simu na picha mjongeo katika ufundishaji wao,” anasema Dk. Lilian.
Dk. Jason Mkenyeleye ni mhadhiri mwandamizi Idara ya Hisabati na Takwimu Chuo Kikuu cha Dodoma, anayeeleza kuwa mafunzo hayo yameboresha mbinu za ufundishaji za walimu ikilinganishwa na hali ilivyokuwa awali.
Anasema walimu sasa wana uwezo wa kuandaa na kutekeleza shughuli zao kwa kutumia zana za kisasa, kulingana na mabadiliko ya mitaala, pamoja na kuzingatia matumizi ya TEHAMA.
CHANGAMOTO
Anazieleza kuwa ni walimu walioshiriki mafunzo baadhi yao kukosa vifaa vya TEHAMA, jambo linalozuia utekelezaji wa mbinu mpya.
Dk. Mkenyeleye anasisitiza kuwa ni muhimu kwa shule kupata vifaa hivyo kwa wingi, ili walimu wavitumie na mbinu bora za kufundisha.
Mwalimu wa hisabati kutoka Shule ya Sekondari Binza, mkoani Simiyu, Mzee Luchagula, anasema wamejifunza mbinu za kisasa za ufundishaji, zikiwamo matumizi ya teknolojia, ambazo zitawawezesha kushirikisha wanafunzi zaidi darasani.
Anaongeza kuwa, kwa kutumia mbinu hizo, wamepata uwezo wa kumudu darasa lenye wanafunzi wengi kwa kutumia teknolojia na kukabili ulemavu alionao.
Thimon Baitu, anayefundisha fizikia katika Shule ya Sekondari Meatu, mkoani Simiyu, anasema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua umuhimu wa kutumia TEHAMA mfano video za msisimko wanapofundisha.
Anasema kwa kufanya hivyo, wanafunzi wataelewa kwa urahisi mada za fizikia, ingawa anaitaja changamoto ya kukosa vifaa vya TEHAMA na intaneti kuwa kikwazo.
Mwalimu wa Hisabati Sekondari ya Busangwa, Fathiya Shah, anaeleza kufurahia mabadiliko ya mitaala ambayo yamewezesha walimu kujifunza TEHAMA kufundisha.
“TEHAMA, itawasaidia wanafunzi kuelewa vizuri hisabati kwa njia ya vitendo, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wakitegemea nadharia pekee,” anasema.
Kutoka Sekondari ya Nkololo, mkoani SImiyu, mwalimu Nyandamboje Lulyalya, anayeishi na ulemavu anasema mafunzo hayo yamempa ujuzi wa kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira yake kufundisha kwenye maabara.
Anasema mbinu za kufundisha kwa kushirikisha wanafunzi zitaongeza ufanisi katika kujifunza kemia.
Aidha, anataja ukosefu wa vifaa na ujuzi wa walimu kufundisha somo hilo kwa vitendo kuwa ni changamoto, akiomba mafunzo hayo kuendelea ngazi ya wilaya ili walimu wengine wanufaike.
Mdhibiti Ubora kutoka Wilaya ya Rorya, Masanja Mashimba, anaongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia walimu kutumia mbinu za kisasa na kusimamia ufundishaji bora.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED