Trump kutinga tena Ikulu kibabe Jumatatu saa sita mchana

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 08:10 AM Jan 15 2025
Trump kutinga tena Ikulu kibabe Jumatatu saa sita mchana.
Picha: Mtandao
Trump kutinga tena Ikulu kibabe Jumatatu saa sita mchana.

WIKI ijayo inaweza kuitwa ni ya Donald Trump. Kwani kile alichokitaka amekipata. Ni urais wa Marekani anaoupambania kwa nguvu zote, licha ya wabaya wake kutishia kumuua kwa risasi akiwa jimboni Pennsylvania, wakati wa kampeni.

Anakula kiapo Jumatatu ijayo. Anatinga ikulu akiwa Rais wa Marekani wa 47. Anaingia na historia ya kuwa rais wa pili kurudi madarakani katika vipindi visivyofuatana.

Jarida la Times Magazine la Marekani linabainisha hayo, kwamba Trump na Grover Cleveland, ndiyo marais pekee nchini humo, kuingia madarakani kwa vipindi tofauti visivyofuatana.

Cleveland aliongoza Marekani kuanzia 1885-1889 na kurejea tena madarakani 1893 hadi 1897. Kwa mujibu wa jarida la Times Magazine.

TRUMP

Donald Trump (78), Januari 20, anaapishwa kuwa rais rasmi, akipokea kijiti kutoka kwa Rais Joe Biden. 

Trump alishika mamlaka hayo lakini mwaka 2020 aliwekwa pembeni akiwa rais wa 45 wa nchi hiyo yenye nguvu kiuchumi duniani. 

Zikisalia siku chache, Trump kuingia Ikulu ya White House, inakadiriwa watu kadhaa watahudhuria na mamilioni kushuhudua kupitia vyombo vya habari kwenye mitandao na runinga duniani kote.

Inakadiriwa kwamba watu milioni 31 walijumuika kushuhudia sherehe za kuapishwa kwa Donald Trump Washington D.C., Ijumaa, Januari 20, 2017.

Uapisho wa Barack Obama, muhula wa pili uliofanyika Januari 21, 2013, ulivutia watazamaji milioni 20.55 huko Marekani. Na uapisho wake wa kwanza Obama, watu milioni 38 walishuhudia na kuwa wa pili kufuatiliwa zaidi baada ya ule wa Ronald Reagan, mwaka 1981.

Ingawa kuna maswali ya wadadisi kwamba je, Trump, atavunja rekodi ya Barack Obama, kuwa na wafuatiliaji wengi duniani wakati akiapishwa.

Trump, ambaye alimdhibiti Makamu wa Rais, Kamala Harris katika uchaguzi mkuu wa 2024, alithibitishwa kama mshindi wa uchaguzi huo wakati wa kikao cha pamoja cha Congress, Januari 6, mwaka huu, wiki ijayo anarudi katika Ikulu ya White House.

Kulingana na masharti ya mabadiliko ya 20 ya Katiba ya Marekani, rais mpya anachukua rasmi madaraka saa sita mchana, Januari 20, 2025. Awali rais mpya alikuwa anachukua madaraka Machi 4.

KINACHOJIRI UAPISHO

Rais anayeondoka madarakani, kwa kawaida hutembea pamoja na rais mteule hadi jengo la bunge, kwa ajili ya sherehe ya kuapishwa.

Rais anayeondoka ataacha ujumbe kwenye Ofisi ya Rais anakofanyia kazi na shughuli zake iitwayo Oval Office ili mrithi wake anayeingia kazini ausome.

Kawaida, makamu wa rais hula kiapo chake kwanza, kisha rais mteule anafuata.

Kiapo hicho kinafanyika karibu na saa sita mchana, siku ya kuapishwa, ili kuendana na wakati rasmi rais mpya anapochukua madaraka.

Baada ya viapo vya madaraka, rais mpya hutoa hotuba ya kuapishwa, anaandika masuala yake vya kwanza vya kisheria katika sherehe ndani ya bunge, na kisha anashiriki kwenye maandamano yanayojaa mitaani ya Washington. Umma hukaribishwa kushiriki kwenye tukio hilo kubwa.

MAANDALIZI

Tangu mwaka 1901, Kamati ya Pamoja ya Congress kuhusu sherehe za kuapishwa, imeshughulikia maelezo mengi ya sherehe za rais kuapishwa madarakani.

Kamati hiyo ina wanachama kutoka vyama vya kisiasa vyote vya Marekani. Kundi la mwaka huu linajumuisha Spika wa Baraza la Wawakilishi Mike Johnson, Kiongozi wa Wengi wa Seneti Chuck Schumer.

USHINDI WA TRUMP 

Kinyang'anyiro kati yake na mgombea wa Chama cha Democratic Kamala Harris, kilidhaniwa kuwa cha ushindani mkali lakini matokeo ya uchaguzi yalionesha kuwa Trump amepata kura za kutosha kushinda.

Atakuwa rais wa kwanza wa zamani kurejea madarakani kwa zaidi ya miaka 130, akiwa na miaka 78, kuchaguliwa katika wadhifa huo.

Viongozi wa dunia walipongeza Trump kwa ushindi wa uchaguzi wa rais Marekani miongoni mwao Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na mwenzake wa Uingereza, Keir Starmer. 

Kulikuwa na hofu kwamba ushindani mkali kati ya wagombea katika baadhi ya majimbo muhimu ungeibua maswali mengi kuhusu matokeo ya uchaguzi huo.

Lakini mambo yaligeuka ghafla katika majimbo ya North Carolina, Georgia, Pennsylvania na Wisconsin, pamoja na ushindi katika majimbo ambayo yamekuwa yakiunga chama cha Republican, ulimwezesha Trump kufikia idadi ya kura 270 ya wawakilishi maalum wanaohitajika kushinda uchaguzi wa urais.

Trump sasa ni rais mteule, na mgombea mwenza wake James David Vance au JD Vance anakuwa makamu wa rais mteule, ambao watakuwa viongozi rasmi Jumatatu ijayo. Baada ya kuapishwa, rais mpya anaanza kazi mara moja. 

Kabla ya kuapishwa, Rais mteule Trump na makamu wa rais mteule JD Vance, watafanya kazi na timu yao ya mpito kuandaa makabidhiano hayo kutoka kwa utawala wa Rais Biden.

Walianza kubainisha vipaumbele vyao vya sera, kuanza kuhakiki wagombeaji ambao watachukua majukumu muhimu katika utawala mpya, na kujiandaa kuongoza serikali.

Trump na timu yake pia walianza kupokea taarifa za siri za usalama wa taifa zinazohusu vitisho vya sasa na operesheni zinazoendelea za kijeshi.

Rais mteule na makamu wake pia wanapata ulinzi wa lazima kutoka kwa idara ya huduma ya usalama (Secret Service) ya Marekani.

Aidha, anayeondoka kwa kawaida humwalika rais mteule katika Ikulu siku chache baada ya uchaguzi.

Pia kwa kawaida huhudhuria hafla ya uapisho wake kuashiria makabidhiano ya madaraka kwa amani, ingawa Trump aliamua kususia hafla hiyo mwaka 2020.

Hata hivyo alifuata desturi iliyoanzishwa na Ronald Reagan ya kuacha barua iliyoandikwa kwa mkono katika Ofisi ya Oval, ili mrithi wake aisome.

Wakati huo, Rais Biden aliwaambia waandishi wa habari kwamba mtangulizi wake alikuwa ameacha "barua ya ukarimu sana".