Programu ufanisi wa nishati kuleta mabadiliko ya kisekta

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 12:00 PM Nov 12 2024
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Wilson Nyamanga, akikabidhi cheti kwa mwanafunzi aliyepata ufadhili wa masomo ya ufanisi wa nishati katika DIT kwa msaada wa UNDP, EU, na Ubalozi wa Ireland.
Picha: Maulid Mmbaga.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Wilson Nyamanga, akikabidhi cheti kwa mwanafunzi aliyepata ufadhili wa masomo ya ufanisi wa nishati katika DIT kwa msaada wa UNDP, EU, na Ubalozi wa Ireland.

PROGRAMU ya ufanisi wa nishati italeta mabadiliko ya kisekta nchini katika kuimarisha mifumo ya kisheria, udhibiti, kitaasisi, kiutawala, kutoa usaidizi kwa watumiaji wakubwa, wa jumla, ukuzaji wa uwezo na ujuzi kwa vijana.

Progaramu hiyo pia inalenga kuongeza uelewa wa umma na mwonekano wa manufaa ya kiuchumi, kifedha, kimazingira na kijamii ya ufanisi wa nishati na nishati mbadala.

Hayo yalielezwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Wilson Nyamanga, ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, katika hafla ya utoaji wa vyeti vya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 25 ngazi ya Shahada za Uzamili katika Uhandisi wa Nishati Endelevu, iliyofanyika juzi mkoani Dar es Salaam.

“Mpango wa utekelezaji wa ufanisi wa nishati, ambao tunatekeleza, umeundwa ili kuziba pengo la kijinsia katika sekta ya nishati, kwa kuweka kipaumbele katika ukuzaji wa ujuzi na sifa za kitaaluma katika usimamizi na ukaguzi wa nishati.

“Kuwawezesha wataalamu zaidi, hasa wanawake, kuwa na ujuzi katika maeneo haya kwa kutambua kwamba wafanyakazi wenye ujuzi ni muhimu katika kuendeleza malengo ya ufanisi wa nishati ya Tanzania na kukuza maendeleo endelevu katika sekta nzima,” alisema Nyamanga.

Aliongeza kuwa mpango huo kwa awamu ya kwanza ulichukua wanafunzi wanawake 10 na hadi sasa wamefikia 35 hatua itakayosaidia kuleta mafanikio makubwa kuelekea maono yao ya nguvu kazi ya nishati jumuishi.

1

Aidha, alisema wapokeaji wa ufadhili huo wanawakilisha mustakabali wa sekta ya nishati, na mafanikio yao yatachukua jukumu muhimu katika kuunda mazingira endelevu na jumuishi ya nishati katika taifa.

Alisema hivi karibuni watazindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Jadidifu na Mkakati wa Kitaifa wa Ufanisi wa Nishati ambao ni muhimu kwa mustakabali wa nishati ya Tanzania na mafanikio yake yatategemea wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu.

Kaimu Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Muyeye Chambwera, alisema kukuza usawa wa kijinsia katika sekta ya nishati si tu suala la usawa ni mkakati madhubuti wa kufikia Malengo Maendeleo Endelevu (SDGs), hasa (SDG 5) kuhusu usawa wa kijinsia.

“Pia utasaidia kufikia malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 7) kuhusu nishati nafuu na safi. Mitazamo na utaalamu wa kipekee wa wanawake ni muhimu kwa ajili ya kuendesha uvumbuzi na kukabiliana na changamoto tata tunapojitahidi kukidhi mahitaji ya nishati ya Tanzania kwa uendelevu,” alisema Chambwera. 

Programu hiyo inatekelezwa katika Taasisi ya Teknolojioa Dar es Salaam (DIT) chini ya ufadhili wa UNDP Tanzania, Umoja wa Ulaya (EU) na Ubalozi wa Ireland.

2