SERIKALI ya Mkoa wa Mwanza imekikabidhi Chama Kikuu Cha Ushirika Nyanza (NCU 1984), zaidi ya Sh. bilioni 1.8 zilizokuwa zimehifadhiwa katika akaunti maalum.
Akizungumza jana jijini hapa katika hafla ya makabidhiano ya fedha hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alisema, fedha zilikuwa zimehifadhiwa katika akaunti hiyo iliyofunguliwa mwaka 2018.
Alisema fedha hizo zaidi ya Sh.bilioni 1.8 zilitokana na makusanyo ya mali mbalimbali za NCU 1984, zilizorejeshwa na serikali kutoka kwa watu waliokuwa wakizimiliki kinyume na utaratibu.
"Baada ya kurejeshwa kwa mali hizo, Ofisi ya Waziri Mkuu iliyokuwa ikiratibu ilielekeza kufunguliwa kwa akaunti maalum iliyokuwa ikisimamiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kipindi cha mpito, wakati mchakato wa kurejesha umiliki wa mali hizo kwa NCU ukiendelea," alisema Mtanda.
Alisema, kwa kipindi chote serikali ya mkoa ilikuwa ikisimamia akaunti hiyo maalum ya NCU 1984 hadi Aprili 5, mwaka huu, ilikuwa na salio la zaidi ya Sh. bilioni 1.858 nao mkoa una matumaini fedha hizo zitatumika kukiimarisha chama hicho na wanachama wake.
Naibu Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) Collens Nyakunga, kwa niaba ya Mrajisi Mkuu wa Ushirika alisema, NCU 1984, ilikuwa ikidaiwa na Benki ya CRDB Sh. bilioni 2, lakini benki hiyo ilichukua mali zilizozidi fedha ilizokuwa ikidai.
Alisema CRDB walichukua mali ya bilioni 16 wakati deni ni Shilingi bilioni mbili na serikali ilibaini mali tisa zilizokuwa zikimilikiwa na NCU zilitaifishwa bila utaratibu, zikiwamo za kiwanda cha New Era Oil Mill, jengo la KAUMA, Kiwanda cha Mkonge na viwanja vyake vitatu.
"Pia kuna kiwanda cha Ashok na viwanja vyake 12, ghorofa ya kuishi na nyumba nyingine zilizopo Isamilo, hivyo mali zilizorejeshwa zina thamani ya Sh. bilioni 61.3," alisema Nyakunga.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED