Biashara Soko la Kariakoo sasa saa 24

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 11:47 AM Dec 24 2024

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Picha:Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kuanzia Januari mwakani shughuli za ufanyaji biashara katika Soko la Kimataifa la Kariakoo jijini Dar es Salaam zitakuwa wazi kwa saa 24.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali.

Chalamila alisema uzinduzi rasmi kwa ajili ya kuanza utaratibu huo wa biashara katika soko hilo utafanyika mwanzoni mwa mwaka 2025.

Alisema tayari serikali imeanza kuboresha miundombinu ya soko hilo ikiwa ni pamoja na kuweka kamera za usalama, taa za barabarani na vifaa vingine muhimu ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa.

“Dar es Salaam ina uwezo wa kuendesha biashara saa 24, Kariakoo kama soko linalohudumia mataifa jirani, litachangia kuimarisha uchumi wa mkoa na kuongeza nafasi za ajira,” alisema Chalamila.

“Na tunataka mpango huu utumike kuimarisha amani na kuboresha Jiji la Dar es Salaam kama kitovu cha biashara kwa nchi jirani kama Rwanda, Burundi, Comoro na Uganda.”

Kadhalika, alisema katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu, alisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama ili kudumisha amani.

Alisema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha usalama wa wananchi unaimarishwa katika kipindi chote cha sikukuu na kutoa wito kwa wananchi kutembea na vitambulisho ili kurahisisha utambuzi wao katika matukio ya dharura.

Kadhalika, aliwataka wananchi kuepuka kusambaza uvumi usio na msingi kwa sababu kufanya hivyo wanasababisha taharuki kwenye jamii.

“Niwaonye wananchi katika mkoa huu wa Dar es Salaam, waepuke kusambaza taarifa za uvumi zisizo na msingi, taarifa zisizo sahihi zinaweza kusababisha hofu isiyo na lazima na kuathiri usalama kwa jamii,” alisema Chalamila.

Pia, aliwapongeza waandishi wa habari kwa mchango wao katika kufikisha taarifa kwa jamii na kusaidia kujenga taifa kupitia ukosoaji wenye lengo la kujenga na kuwahimiza kuwa waangalifu na taarifa wanazozitoa, hususani zinazohusu matukio ya utekaji akisisitiza umuhimu wa kuthibitisha usahihi wa taarifa kabla ya kuzisambaza.

Vilevile, alitoa angalizo za usahihi na kuthibitisha taarifa zinazotolewa akirejea taarifa za matukio ya utekaji zilizoripotiwa hivi karibuni.