NBC yapewa Tuzo ya Uwajibikaji Bora kwa Jamii

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:31 PM Jul 23 2024

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC, Theobald Sabi akionesha tuzo ya Benki Bora Tanzania kwa Uwajibikaji wa Jamii kutoka Tuzo za Ubora za Euromoney 2024.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC, Theobald Sabi akionesha tuzo ya Benki Bora Tanzania kwa Uwajibikaji wa Jamii kutoka Tuzo za Ubora za Euromoney 2024.

Benki ya NBC imetangazwa kuwa Benki Bora ya Tanzania katika eneo la Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika Tuzo za Ubora za Euromoney 2024. Utambuzi huu unaakisi dhamira ya benki hiyo katika uwezeshaji wa kiuchumi na kijamii katika jamii inayohudumia.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC, Theobald Sabi, ametoa shukrani kwa tuzo hiyo na kusisitiza jukumu la benki kama mtoa suluhisho na uwezeshaji wa jamii na ukuaji wa kiuchumi. Ikiwa na kauli mbiu "Conveniently Everywhere,"  (Kwa Urahisi kila Mahali)  benki hiyo inatoa mfumo wa huduma za kifedha kwa njia za kawaida  na kidijitali kufikia mahitaji ya wateja na kuboresha ustawi wao wa kiuchumi na kijamii.

"Kutangazwa kuwa Benki Bora ya Tanzania kwa Uwajibikaji wa Jamii ni ushahidi wa dhamira yetu ya kuwa na athari chanya katika jamii," alisema Sabi. "Tunaamini katika kuwapa nguvu jamii zetu na kuchangia maendeleo  yao endelevu. Utambuzi huu unatuhamasisha kuendelea kujenga Tanzania bora."

Sabi ameelezea mchango mkubwa wa Benki ya NBC katika elimu, afya, uanzishaji wa biashara kwa vijana, na uhifadhi wa mazingira. Ripoti yao ya Uendelevu ya 2023 inaonesha mchango wa katika mazingira, kijamii na na dhamira yao endelevu katika jitihada mbalimbali za kimaendeleo

"Dhumuni letu la kutoa kipaumbele kwa jamii tunayoihudumia ndiyo kiini cha dhamira yetu ya maendeleo endelevu. Hiyo ndio sababu tumetekeleza miradi mbalimbali katika maeneo kama elimu, afya, na uhifadhi wa mazingira," amesema Sabi.

Utambuzi wa benki ya NBC  kwenye tuzo hiyo unajumuisha vigezo kadhaa ikiwemo mwenendo wake katika kufanya biashara kwa kuzingatia misingi ya maadili, ubunifu unaolenga jamii, jitihada za ujumuishaji wa kifedha, na miradi ya mazingira. Bidhaa zao za kibenki kama NBC Shambani, Kuanasi, Wafugaji Account, na Johari Account zimechochea kasi ya  ujumuishaji wa kifedha. Zaidi ya hayo, miradi kama NBC Business Clubs, NBC Dodoma Marathon, NBC Mobile Clinic, Wajibika Scholarships, na mafunzo kwa vijana imekuwa na athari kubwa kijamii.

"Tunajivunia mafanikio yetu katika kuendeleza ujumuishaji wa kifedha na kusaidia maendeleo endelevu," alisema Sabi. "Miradi yetu imekuwa na athari chanya kijamii, na zaidi tunadhamiria kuendelea kuwa na mchango zaidi kwa jamii yetu."

Jitihada za Benki ya NBC zimeongeza athari chanya kwa kijamii. Benki hiyo imesharikiana na  Taasisi ya  Saratani ya Ocean Road kuchunguza saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake 45,000. Benki hiyo pia imewapa ufadhili wa masomo wakunga 100 kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation na kutoa ufadhili wa masomo ya ufundi stadi kwa wanufaika  1,000 kupitia mpango wake wa ufadhili wa masomo hayo unaofahamika kama Wajibika. Zaidi pia benki hiyo imekuwa ikitoa nafasi za kujifunza kwa vitendo kwa wahitimu wa taaluma mbalimbali.

Zaidi benki hiyo imepiga hatua kubwa katika utoaji wa elimu ya kifedha. Zaidi ya wanawake na vijana milioni 1 wamepokea elimu ya kifedha kupitia NBC Business Club, huku wajasiriamali wadogo na wa kati  zaidi ya 20,000 wakipatiwa mafunzo ya ujasiriamali. Washiriki pia walikuwa na fursa ya kuhudhuria Maonesho ya Biashara ya China Canton ili kuongeza uzoefu wao kibiashara sambamba na kutafuta fursa mpya.

 Mbali na tuzo hiyo, hivi karibuni benki hiyo kupitia tuzo za Benki za EMEA Finance ilipewa tuzo ya utambuzi kama Mkopeshaji Kiongozi Bora wa Mikopo ya Serikali barani Afrika kwa mwaka 2023. Utambuzi huo ulikuwa kwa jukumu lao kama Mkopeshaji Kiongozi aliyeteuliwa katika huduma ya mikopo ya Dola 200 milioni kwa Serikali ya Zanzibar.

"Dhamira yetu ya uwajibikaji wa kijamii na miradi yenye athari chanya imeimarisha nafasi yetu kama benki inayoongoza nchini Tanzania. Tunaendelea kuweka kiwango cha juu cha ufanyaji biashara kwa kufuata misingi ya maadili, ushirikishaji wa jamii, ujumuishaji wa kifedha, na uendelevu wa mazingira. Kwa kujitolea kwetu kujenga Tanzania Bora, Benki ya NBC tunastahili utambuzi huu wa heshima.'' amesema Sabi.