Mgeni ukiingia Zanzibar, bima ya wasafiri inakuhusu

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 03:26 PM Jul 26 2024
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum.
Picha:Mtandao
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum amesema uwepo wa bima ya wasafiri kutaongeza kasi ya idadi ya watalii kufika Zanzibar na serikali kupata mapato yatokanayo na sekta ya utalii.

Aliyasema hayo jana wakati wa utambulisho wa bima hiyo kutoka kwa wadau wa sekta ya usafiri.

Alisema Serikali ya Zanzibar inatarajia kuweka bima ya wasafiri kwa wageni wanaofika Zanzibar ambapo bima hiyo itaanza rasmi mwanzoni mwa Septemba mwaka huu.

Alisema serikali inaendelea na kukamilisha taratibu ya bima hiyo ambao itasimamiwa na Shirika la Bima Zanzibar na itasiadia kuhudumia wageni.

Aidha, alisema pia serikali inaendelea kuboresha miundombinu yao ya kiuchumi pamoja na mifumo ili kuhakikisha wanatoa huduma bora wa wananchi pamoja na wageni.

Hivyo, alisema serikali itajitahidi kuweka miundombinu ambayo itahakikisha wananchi na wageni wanapata huduma bora na wanaendelea na mchakato kuona mambo yao yanakuwa mazuri ili watakapoanza kutumia huduma hiyo kuwe hakuna changamoto.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Jape Ussi Khamis, alisema uwepo wa bima hiyo itachangia utalii kuwa mzuri na Zanzibar kuwa salama kwa watalii wanaoitembelea.

Alisema kuwa serikali inatengeneza mambo mengi mazuri kwa ajili ya uchumi wa Zanzibar na miongoni mwa suala ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi ni sekta ya utalii.

Meneja Biashara, Benki, Bima, Mawakala na Mauzo kutoka ZIC, Hamida Salim  Juma alisema bima ya usaifri ni sawa na bima nyingine ambazo mgeni ataipata akiwa nchini na itaukuza uchumi wao na kuupa tija.

Alisema bima hiyo haitatumika katika masuala ya kiafya pekee bali itatumika kwa majanga yote ambayo watakuwa wanapata wageni hao wakiwa nchini au katika mipaka ya Tanzania.

Alisema utaratibu wa kupata bima hiyo utaanzia tangu mgeni huyo atakapoomba kufika Zanzibar.