Maagizo matano nishati safi ya kupikia

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 05:19 PM Nov 09 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Picha: Bunge
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa maelekezo mahsusi matano kwa taasisi, wizara na umma kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia likiwamo ifikapo mwezi ujao.

Katika kutekeleza hilo, ametaka wakuu wa mikoa na wilaya kuonesha ni taasisi ngapi tayari zimetekeleza agizo hilo.

Akiahirisha mkutano wa 17 wa Bunge jana jijini hapa, Majaliwa alisema taasisi zote zenye kuandaa chakula cha watu zaidi ya 100 zinapaswa kutekeleza maagizo ya kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Wizara ya Nishati iendelee kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia; wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kote nchini, wafanye ukaguzi katika taasisi zilizomo katika maeneo yao mathalani majeshi na polisi.

“Vyuo vya elimu ya kati na ya juu, vyuo vya wizara mbalimbali kama elimu, afya na kilimo, ambapo yanayopaswa kubadilisha mifumo yao ya nishati ya kupikia kwa vile yana idadi kubwa ya walaji wa vyakula,” alisema.

Majaliwa alisema wajasiriamali wanaopika chakula cha watu wengi kama vile katika harusi wahamasishwe ili nao wabadilishe teknolojia zao, ziendane na matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Ninawaelekeza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wote ifikapo mwezi Desemba, mwaka huu, watoe taarifa ya utekelezaji kuonesha ni taasisi ngapi tayari zimetekeleza agizo hili.

“Hii ni kwa taasisi zote za umma na binafsi. Lengo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2033 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ambayo ni: gesi, umeme, vumbi la makaa ya mawe, Kunipoa zinazotokana na takataka,” alisema.

Majaliwa aliwataka wananchi waendelee kubadili mfumo wa maisha hususani taratibu za kupika chakula ili kuachana na nishati chafu ya kupikia inayohusisha kuni na mkaa unaotokana na miti.

Pamoja na hayo, aliagiza wizara zote kuandaa kwa wakati taarifa za utekelezaji wa maazimio yote ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati za Bunge, na kuziwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu ili iweze kuwasilisha taarifa ya serikali kwa Spika wa Bunge.

Pia, aliwataka watendaji wote serikalini wahakikishe vipaumbele vilivyoanishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026 vinatafsiriwa vema kwenye mipango ya taasisi zao.

Majaliwa alisema serikali imeendelea kusimamia makusanyo katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024/25 na Sh. trilioni 11.55 zimekusanywa kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi. 

Alisema mafanikio hayo yanatokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na serikali ikiwamo kuendelea kuimarisha na kuhimiza matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato na kuhamasisha matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki.