Kamati yagoma kukagua ujenzi kituo kisa ukosefu kofia ngumu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:03 AM Nov 10 2024
 Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Justin Nyamoga
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Justin Nyamoga

Kamati ya Bunge Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeshindwa kufanya ukaguzi katika jengo la Kituo cha Biashara Kimataifa linalojengwa Ubungo kutokana na uchache wa kofia ngumu.

Kamati hiyo ikiwa pamoja na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, wabunge na wataalamu walifika katika jengo hilo jana majira ya saa 5:40 kwa ajili ya kufanya ukaguzi kuona maendeleo ya mradi na kutoa ushauri.

Baada ya kufika katika eneo hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Justin Nyamoga, alimtaka msimamizi wa mradi huo awagawie yeye na jopo lake vifaa vya kujikinga na madhara wakati wa kukagua mradi huo ikiwamo kofia.

Hata hivyo, msimamizi wa mradi huo, alisema kofia zilizopo ni chache kwamba zingewatosha wabunge 10 pekee kwa kuwa kuna ugeni ulifika ghafla umetumia kofia hizo na kuharibu bajeti yao.

Hapo ndipo Nyamoga aligeuka mbogo na kuuliza mlikuwa na taarifa ya ugeni huu kwa nini hamkuandaa vifaa?  inakuwaje mradi mkubwa kama huu zikosekane kofia kwaajili ya wageni wa kamati ya bunge? 

 "Kukagua huu mradi bila vifaa vya kujikinga ni kuhatarisha afya za wabunge na wageni wengine" alisema Nyamoga.
 Kutokana na sintofahamu hiyo, wakiwa katika eneo hilo, Nyamoga aliwaita wabunge  kujadili mustakabali wa suala hilo ndipo walipokuja na jibu la pamoja kusitisha ukaguzi mpaka kesho watakapokuwa wamejiandaa vizuri.

 Baada ya kutoka katika mradi huo, Kamati hiyo ilifanya ukaguzi katika barabara za makumbusho ambapo ilimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha taa za barabarani zinakarabatiwa ili jiji liwe jeupe nyakati za usiku.

 Ni maelekezo yaliyoyolewa baada ya kitajwa adha hiyo ni moja ya changamoto zinazoikabili barabara hizo.

 Akiwa katika mradi wa mradi wa biashara DDC unaojengwa kariakoo baada ya kutoka makumbusho aliagiza halmashauri zote nchini kushirikiana na sekta binafsi Katika kufanikisha uwekezaji.

Aliwaomba wadau mbalimbali katika sekta za umma kushirikiana na serikali kuwekeza ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
 Nyamoga alisema huo ni uwekezaji sahihi kwa wakati sahihi na hivyo kamati inatoka maelekezo halmashauri zote zenye fursa zijifunze kwa Jiji la Dar es Salaam katika kutumia maeneo hayo kama fursa.

Aidha aliwataka wasimamizi wa mradi huo kufanya namna bora ya uwazi wakati wa kugawa maeneo hayo mradi utakapokamilika Ili kuepusha migogoro kwa wafanyabiashara.

Alisema Kamati hiyo imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi  akisisitiza anatamani ukamilike haraka ili uweze kusaidia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.