MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametangaza kuanza operesheni ya kubaini wakwepaji kodi na kutoa rai kwa wafanyabiashara kutoa ushirikiano ili jukumu hilo lifanyike kwa urahisi.
Pia ameonya wafanyabiashara kutoingia kwenye mgomo kuzuia zoezi hilo. Kufanya hivyo ni kukiuka 4R za Rais Samia Suluhu Hassan za maridhiano, kujenga upya, kuvumiliana na kustahimiliana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Chalamila alisema lengo la operesheni hiyo ni kuhakiki matumizi sahihi ya mashine za kutoa risiti (EFD) kwenye maduka na maghala na stempu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwenye vinywaji vikali na baridi.
"Kuna kasumba ya kuingiza vinywaji ambavyo havijathibitishwa na mamlaka husika kama ya viwango (TBS) na mamlaka zingine na hata zile zilizozalishwa hapa nchini, zipo ambazo zinauzwa bila stempu za TRA…Huu ni uhujumu wa uchumi wa taifa letu na uhujumu wa afya za Watanzania.
Mchakato tulionao hivi sasa ni kuendeleza operesheni kubwa ili kuwabaini wale wote wanaofanyakazi hizi kwa kuwa lengo lao ni kuhujumu uchumi wa nchi yetu.
"Mara kadhaa tumekuwa tukisikia harufu ya migomo kwa baadhi ya wafanyabiashara na migomo hii huja tu mara TRA inapotaka kuanza kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria katika maghala, maduka au operesheni za kuangalia matumizi sahihi ya EFD.
"Wafanyabiashara wowote watakaoinuka na kuanza kutangaza migomo hii, kwetu kama serikali migomo ni tamko la vita, nitoe rai kwamba Tanzania si nchi ya kivita Tanzania ni nchi iliyosimamia misingi ya maridhiano, kujenga upya taifa letu lakini zaidi kuvumiliana na kustahimiliana,” alisema Chalamila.
Chalamila alielekeza wafanyabiashara wote wa vinywaji baridi na vikali kuhakikisha vinakuwa na stempu halisi za TRA, ili kodi iliyokusudiwa iweze kukusanywa.
"Serikali ipo tayari kuendelea kupokea maoni, kusikiliza na kufanya mabadiliko ya kisheria pale itakapolazimika kufanya hivyo," alisema Chalamila.
Aliieleka TRA kuhakikisha inawasaidia wafanyabiashara ili waweze kufanya kazi zao bila vikwazo vya kikodi.
Wakati huo huo, Chalamila amewataka wafanyabiashara na wakuu wa taasisi mbalimbali kufanya marejesho ya kodi kwa mujibu wa sheria kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
“Mfanyabiashara ni wakala tu wa kukusanya kodi kutoka kwa mwananchi kwenda serikalini, fedha hii inaenda kutoa huduma kwa wananchi. Tunapoelekea mwishoni mwa mwaka wa fedha, tufunge tukiwa tumelipa kodi vizuri ili tuijenge nchi yetu," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED