Tatizo la taa viwanja vya soka mikoani lifanyiwe kazi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:49 AM Mar 11 2024
Uwanja wa Manungu Turiani.
PICHA: MTANDAO
Uwanja wa Manungu Turiani.

BAADA ya idadi kubwa ya mashabiki kuangalia mechi mbili za Simba na Yanga zilizochezwa usiku katika viwanja tofauti vya mikoani, wameonekana kulalamikia taa kuwa zina mapungufu.

Yanga ilicheza dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi Ijumaa iliyopita, kuanzia saa 12:00 jioni, na juzi Simba ilikuwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ikicheza dhidi ya Coastal Union.

Mechi hiyo nayo ilianza saa 12:00, lakini zote hizo zilionekana taa zilizofungwa kwenye viwanja hivyo ni za aina moja.

Na siyo viwanja hivyo tu, binafsi hata ukiangalia taa za viwanja vya Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera, Jamhuri Dodoma, vyote hivyo vinaonekana kuwa na matatizo.

Ni tofauti kabisa ukiangalia mechi Uwanja wa Benjamin Mkapa na ule wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Ubora wa taa za viwanja hivyo viwili, au mtu aliyezoea kuangalia mechi kwenye viwanja hivyo, wala hatotumia ujuzi wowote kung'amua kuwa kuna tofauti ya ubora wa taa.

Nikisema hivyo sina maana kuwa waliokuwa uwanjani hawaangalii vizuri mpira, au wachezaji ndani wanashindwa kucheza ama kuna maeneo hawaoni, la hasha.

Tatizo la taa linaloonekana ni kwa wale walioangalia mechi kupitia televisheni. Hawa ndiyo wanaathirika mno na mechi zinazochezwa kwenye viwanja vya mikoani.

Kwa kiasi kikubwa watazamaji wanachoona zaidi ni wachezaji kuliko mpira. Huonekana tu pale wachezaji wanapovutwa na kuonekana wakubwa.

Kasheshe ni pale wachezaji wanapokuwa kwenye saizi ya kwaida ya kuonyesha mpira kama ilivyozoeleka, mpira hauonekani, unachoweza kuona wachezaji wanakimbiakimbia.

Watazamaji sasa wanakuwa wanamtegemea zaidi mtangazaji ili kujua mpira uko wapi, kama umeshapigwa krosi, shuti, umeokolewa au kipa kadaka.

Narudia tena, hili huwezi kuliona kwenye viwanja wa Benjamin Mkapa au Azam Complex, hata mpira ukichezwa usiku wa manane.

Binafsi, nimeliona hilo, lakini hata mashabiki wengi wameonekana kulalamikia hilo, hivyo naliwasilisha kwa wahusika ambao ni Bodi ya Ligi nchini, TPLB.

Inaonekana kabisa kuwa aina ya taa zilizofungwa, pamoja na dhamira njema, lakini wataalam hawajaangalia kama zinaweza kuoana na miale ya taa zingine zilizopo kwenye televisheni za majumbani na mionzi yake inapokutana na macho ya binadamu.

Kuangalia soka ni burudani, ambapo kwa sasa limebeba mashabiki wengi, wake kwa waume na watoto, hivyo kasoro kama hizi ni lazima ziangaliwe na kurekebishwa mbele ya safari.

Nimeona baadhi ya wachambuzi walikuwa wakiorodhesha kasoro mbalimbali kwa wenye mamlaka ya kuonyesha mpira kwenye televisheni, ikiwamo picha za marudio, engo za kukaa na vitu vingine vya kiufundi kwa hiyo wakati hayo yakifanyiwa kazi, na hili suala la taa nalo liangaliwe kwani linakera.

Kwa Watanzania wengi ambao wamezoea kuangalia mechi mbalimbali za ligi barani Ulaya ambapo mpira unaonekana mpaka nembo yake, achilia mbali ubora wa taa za uwanjani na uonyeshaji wenyewe, leo wanakutana na mechi inayochezwa Mkwakwani au Majaliwa, halafu anaona watu tu wanakimbia, mpira wenyewe hauoni, sidhani kama atafurahi.

Kama tunasema Ligi ya Tanzania ni namba sita kwa sasa kwa ubora Afrika, basi kuna vitu vingi vya kuvitazamani ikiwamo ubora wa taa zetu za uwanjani.

Nafikiri pia walioweka taa hizo ndiyo hawa hawa ambao wamedhamini ligi kwa kuionyesha, hivyo kuna vitu vya kitaalam vya kufanya ili mechi zinazochezwa usiku zionekana katika ubora unaotakiwa na isiwe kama mpira wa vikatuni.