MATUMIZI ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), yaliyoenea dunia nzima, ni hatua muhimu ya kuenea lugha mbalimbali zikiwamo za kimataifa na kikanda.
Kwa sasa, lugha nyingine za Kiafrika mfano Kiswahili kinachozungumzwa karibu ukanda wote wa Afrika Mashariki , Kusini na Kati, Kichewa kinachotumika na raia wengi wa Zambia, Zimbabwe na Malawi ni miongoni mwa zile zinazosambaa kwa kasi.
Kiswahili kimeenea kikitumiwa na walimu katika kufundisha na kujifunza kwenye baadhi ya shule na vyuo vikuu sehemu nyingi duniani, mfano Afrika Mashariki, China na Marekani.
Lugha hii ya taifa, imekuwa na umuhimu katika ufundishaji na ujifunzaji wa TEHAMA, kwa sababu inawarahisishia walimu na wanafunzi kuielewa vizuri teknolojia hiyo kwa lugha waliyoizoea.
Hivyo, ninaamini kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kutumia lugha hiyo, katika TEHAMA, kwani ni njia inayoweza kumfanya mwanafunzi afurahie somo kwa kujifunza kwa lugha anayoielewa kwa ufasaha.
Ikumbukwe kuwa lengo la kuanzisha somo la TEHAMA ni kumwezesha mwanafunzi kuimarisha mbinu zake za kupata habari na mawasiliano yaliyoboreshwa katika kujielimisha na kujiendeleza kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa kutumia teknolojia ya asili na ya kisasa.
Hivyo, uamuzi wa kutumia Kiswahili kufundishia, ninaamini unaweza kuleta manufaa makubwa, sio tu katika kuendeleza Kiswahili kama lugha ya taaluma, bali pia kuboresha TEHAMA.
Serikali imekuwa ikigawa vifaa vya TEHAMA, vikiwamo vishikwambi, kwa walimu wote na kuwapa mafunzo ya jinsi ya kuvitumia ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Ninaamini kwamba, katika ulimwengu wa sasa wa maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji ni nyenzo muhimu itakayorahisisha utoaji elimu bora.
Vilevile, matumizi ya Kiswahili kufundishia stadi za msingi za TEHAMA, ni hatua ya mwanzo kuelekea kwenye matumizi ya lugha ya Kiswahili kutolea mafunzo ya kiufundi.
Somo la TEHAMA lilianzishwa katika mtaala mpya wa Elimu ya Msingi (Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, 2005), ili kumpa mwanafunzi maarifa na stadi za matumizi ya habari, vyombo vya mawasiliano.
Hivyo, kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia somo la TEHAMA ni kukifanya kuwa nyenzo ya kuwasilishia elimu ya sayansi na teknolojia ya kisasa, kwani lengo ni kuwasilisha stadi, mielekeo ya maarifa ambayo yamekusudiwa kwa kutumia lugha hiyo ya taifa.
Jambo la muhimu, ni serikali kuendelea kuandaa mafunzo ya kuwajengea walimu uelewa zaidi wa matumizi sahihi ya vifaa hivyo vya TEHAMA ili nao wawafundishe wanafunzi kwa ajili ya kuandaa wataalam wengi wa baadaye wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Lakini pamoja na hayo, kumekuwapo na taarifa kwamba vifaa vingi vya TEHAMA katika baadhi ya shule za msingi zilizowahi kuboreshwa na kuwekwa vifaa hivyo, haviko katika hali nzuri.
Inaelezwa kuwa hali hiyo inatokana na utunzaji wa vifaa hivyo kutokuwa mzuri lakini pia watumiaji wake kutokuwa makini na hivyo kusababisha viharibike mapema vingali vipya.
Ninadhani ingekuwa ni vyema, wakati Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiendelea na mchakato wa kununua vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya vituo vya walimu na vingine maalumu vitakavyochaguliwa kutumiwa na walimu kwenye ufundishaji na ujifunzaji ili kurahisisha utoaji elimu bora na yenye ufanisi nchini, vilivyopo vingetunzwa vizuri.
Kwa kuwa serikali inazidi kuboresha sekta ya elimu ikiwamo kujenga na kukarabati miundombinu kuanzia madarasa, nyumba za walimu na ofisi za walimu, kutoa mafunzo kazini kwa walimu na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ninadhani tatizo hilo pia litashughulikiwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED