Kamati, bodi zimalize kero ya uhaba wa vyoo shuleni

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 05:40 PM Apr 02 2024
Matundu ya vyoo.
PICHA: MAKTABA
Matundu ya vyoo.

UHABA wa matundu ya vyoo ni kero inayoendelea kuzikumba shule za msingi na sekondari, licha ya jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika kunusuru wanafunzi kutoka mazingira hayo hatarishi.

Kwa muda mrefu vyombo mbalimbali, hasa vya habari vimekuwa vikiripoti kuwapo kwa uhaba lakini pia na ubovu wa vyoo katika shule za msingi na sekondari.

 Mfano, Februari mwaka huu, vyombo vya habari viliripoti uhaba wa matundu vya vyoo katika Shule ya Msingi Kahama, katika Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.

Inaelezwa, shule hiyo ina wanafunzi 1,963 na matundu 15 ya vyoo, na kwamba uhaba huo unasababisha wanafunzi 130 kutumia tundu moja la choo kwa siku.

Katika maeneo mengine ya nchi, inaelezwa kuwa baadhi ya shule zina uhaba huo unaosababisha wanafunzi kujisaidia vichakani au katika vyoo vya nyumba za jirani na shule.

Kwa ujumla zinatajwa shule nyingi zina tatizo, ambalo wakati mwingine ni hatari kwa afya za wanafunzi, pia usalama wao, hasa vyoo vyenye nyufa.

Katika mazingira hayo ya uhaba wa vyoo, baadhi ya wanafunzi wanaripotiwa kujisaidia choo kimoja na walimu wao, kitendo ambacho kimsingi hakiko sawa.

Nadhani ni hali inayoweza kurudisha nyuma juhudi za walimu kutoa taaluma, kwani ni vigumu kwa mtoto kujifunza katika mazingira hayo.

Ingekuwa  vyema sasa kuwapo kampeni maalum ya kuhakikisha kila shule inakuwa na matundu ya kutosha, ili kuondoa adha kwa wanafunzi na walimu.

Tunaambiwa kuwa kampeni ya 'nyumba ni choo' imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuhamasisha wananchi kuwa na vyoo vya kisasa, ninadhani kampeni hiyo ingehamia shuleni.

Ikumbukwe tatizo la uhaba wa vyoo sasa limeota mizizi katika shule za msingi na sekondari, ni wazi hazina vyoo vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi.

Hivyo, ni vyema kampeni hiyo ingetua shuleni ili kamati na bodi za shule zihamasike na kuona umuhimu wa shule kuwa na vyoo vya kutosha na tena bora.

Shule hizo ni za umma, ambazo hakuna budi kuzihudumia kadri inavyowezekana, kuanzia chakula cha wanafunzi na hata ujenzi wa miundombinu, ikiwamo ujenzi wa vyoo na hata madarasa.

Kamati na bodi ndizo zinazopanga kuboresha shule kwa kushirikisha wananchi ili waweze kuzihudumia badala ya kujiweka pembeni na kudhani hawahusiki.

Sidhani kwamba ni kosa  wananchi kuchimba mashimo ya vyoo, kufyatua matofali na  kujenga na kwa ajili ya watoto wao.

Cha msingi ni kuimarishwa mfumo wa  ushirikishaji wa wananchi kwa mambo ambayo yanawahusu, ili nao wawe na mchango.

Binafsi ninaamini kwamba ujenzi wa vyoo vya shule umo ndani ya uwezo wa umma si wa kutafuta au kusubiri wafadhili. Jambo la muhimu ni ushirikishaji.

Umma au jamii inapaswa kujishughulisha na tatizo la wanafunzi kukosa vyoo,kupitia kamati na bodi za shule, huku serikali ikitia msukumo.

Kamati na bodi za shule zikifanya sehemu yake ya kushirikisha na kuhamasisha wananchi, huku serikali nayo ikitia msukumo, tatizo la uhaba wa vyoo au shule kuwa na vyoo vibovu linaweza kuwa historia.

Ikumbukwe kuwa, majukumu ya kamati na bodi za shule ni pamoja na kuandaa mipango ya maendeleo ya shule, kuhakikisha shule inakuwa na miundombinu na vifaa kamili na bora.

Vilevile, ni kutafuta vyanzo vya fedha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya shule, hivyo ukubwa wa tatizo la vyoo katika shule za msingi na sekondari linaweza kuisha iwapo kamati na bodi zitawajibika vizuri.

Hapa kinachohitajika ni ubunifu na weledi wa kutatua kero za uhaba zinazozikabili shule badala ya kusubiri fedha kutoka serikalini, huku wananchi wapo ambao ndio wenye shule.

Kamati na bodi zinaweza kubuni vyanzo vingine vya mapato, ili kuboresha miundombinu ya shule, lakini pia wakati mwingine inawezekana kutatua tatizo kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika mazingira husika kama miti, mchanga na mawe na rasilimali watu kumaliza tatizo hilo sugu.

Aidha, kamati na bodi zinaweza kutoa elimu  kwa wanajamii ili itambue shule za umma ni mali yao, hivyo wazihudumie kadri inavyohitajika badala ya kuachia serikali jukumu hilo.