Jamii inahitaji elimu, hatua zaidi kuepuka janga la moto

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:44 AM Oct 24 2024
Jamii inahitaji elimu, hatua

zaidi kuepuka janga la moto
Picha:Mary Kadoke
Jamii inahitaji elimu, hatua zaidi kuepuka janga la moto

HADI sasa elimu ya kukabiliana na majanga inatakiwa kutiliwa mkazo katika jamii, ili kunusuru vifo vya watu na uharibifu wa mali zao.

Kila mara imekuwa ikiripotiwa matukio ya watu kufa kwa kusombwa na maji, ajali, vyombo vya moto, nyumba kuungua na wengine kuangukiwa na kuta.

Wananchi wamekuwa wakiitupia lawama serikali na mahsusi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ikidaiwa kushindwa kunusuru wakati wa majanga hayo yanatokea.

Ila kuna ushahidi wa wengi, kuwapo ujenzi holela wa makazi, ambao nao unachangia maafa hasa ya moto.

Kunashuhudiwa mahali hapo hakuna barabara za kupitisha magari ya jeshi hilo, kupeleka maji ya kuzimia moto na wataalamu husika kutumika inavyopaswa kwa ujuzi na nyenzo nyingine walizo nazo. 

Kinyume chake, kila kunapozuka moto, wakazi wake wamekuwa wakitumia mchanga na maji kuzima moto, bila ya mafanikio. Hiyo ni kutokana na kukosa elimu sahihi ya kukabili janga hilo.

Vilevile, wakati wa mvua, mafuriko yamekuwa yakisababisha madhara kwa jamii tajwa jirani.

Ni aina ya madhara yanayowagusa  watu, hususani watoto wanasombwa na mafuriko, wanakutwa wameshakufa.

Vilevile majanga ya vifo kwa watu kutumbukia visimani, madimbwi na mashimo ya vyoo, tahadhari ingeweza kuchukuliwa endapo jamii ingepata elimu sahihi.

Ni kawaida kukuta choo kina nyufa, hali kadhalika madimbwi, mito kujaa, lakini watu wanashindwa kuchukua tahadhari, wanaendelea kutumia kukumbwa na mkasa wa maafa.

Kimsingi, hiyo ni mifano michache, ila kuna mingi inapatikana kwenye makazi ya watu.

Inashauriwa kabla ya kuanza ujenzi wa makazi kupeleka ramani za nyumba katika mamlaka ya kitaalamu kisheria ya ujenzi, kwa ajili ya ushauri wa namna ya kukabiliana na majanga hayo, ili wapatiwe msaada sahihi.

Ushauri huo ni pamoja na ujenzi wa nyumba kwa mpangilio, unaotoa fursa kwa watu kupita na magari ya zimamoto kwenda kuokoa, panapokuwapo hitaji.

Ukweli ulioko ni kwamba, nyumba nyingi zimekuwa zikitetekea na watu wengi kufia ndani, kwa kukosa msaada wa kikosi hicho cha kuzima moto na uokoaji, kutokana na magari husika kukosa barabara ya kupita hadi kwenye tukio stahiki.

Kinachofanyika mara nyingi, ni kwa baadhi ya wajuzi na wahusika wa tukio  kuamuru umeme uzimwe, ili kudhibiti moto kusambaa kwenye majengo mengineyo, hata yakaleta madhara zaidi. 

Hiyo yote inatokana na uhalisia nyumba nyingi ziko katika maeneo yasiyopimwa na kimsingi, baadhi zipo katika maeneo yaliyoachwa wazi kwa huduma maalum, baada ya viwanja kupimwa,  mathalan mahsusi kwa kupitisha maji wakati wa mvua.

Iko busara ya kukubaliana na ukweli kwamba, pamoja na serikali kuwekeza fedha nyingi kukabiliana na majanga ya namna hiyo, pia jamii inapaswa kuweka mkazo kwenye utoaji elimu ya umma, kuzingatia kanuni na taratibu za miundombinu wakati wa ujenzi wa nyumba zao.

Hata kwa maeneo yasiyopimwa, vilevile kuna mkondo wa kisheria unaomtaka mjenzi kupata kibali cha serikali ya mtaa husika. Hapo kunakuwapo maelekezo ya kufanikisha kwa usahihi na kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia ardhi nchini.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amesikika akizungumzia kuwapo mpango unaotengeneza utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi, kuhusu kinga na tahadhari ya moto.

Kinachodhamiriwa hapo ni kuwawezesha kuwa sehemu ya jitihada za kudhibiti majanga hayo nchini.

Masauni anaitaja kuwa elimu inayowasaidia wananchi kuzuia kutokea moto unaowaachia watu vifo, ulemavu na uharibifu wa mali kwa watu.

Anasema hata yanapotokea majanga ya moto na ajali, wananchi wenye elimu sahihi wanaweza kutoa ushirikiano chanya kwa askari Jeshi la    Zimamoto na Uokoaji.

Mpango wa jeshi hilo unatajwa ni kutoa elimu sahihi kwa wananchi, hali inayowasaidia kupunguza moto na majanga mengine ya namna hiyo kwenye makazi, ajali za barabarani na majini.

Elimu hiyo pia inatajwa kusaidia kunusuru mashamba makubwa ya miti kwa ajili ya biashara na usalama wa mazingira, pia mazao, hata magari yanayonusuriwa kuteketea kwa moto.