Foleni Dar zipatiwe ufumbuzi, zinakwamisha maendeleo yetu

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:51 AM Oct 25 2024
Foleni
Picha: Mtandao
Foleni

DAR ES SALAAM ni mji mkubwa wa kibiashara, pilika ni nyingi, likiongoza kwa idadi kubwa ya watu nchini, kwa kuwa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, inaitaja kuwa na zaidi ya watu milioni tano.

 Ukubwa wake ni mithili ya majiji mengine na miji, linakumbwa na foleni kubwa za magari barabarani ambayo ni kero kwa abiria na watumiaji wengine wa barabara na vyombo vya usafiri kwa ujumla.
 
 Katika mazingira hayo ya foleni, watu wanachelewa kufika kwenye shughuli za uzalishaji mali, wengine hujikuta wakiwa katika hatari ya kupata adhabu za makazini, kutokana na kuchelewa kazini kila mara.
 
 Inaelezwa kuwa foleni hiyo husababisha hasara takribani Sh. bilioni 500 kila mwaka, fedha ambazo zingejenga shule za kisasa 833. Ndivyo Rais Samia Suluhu Hassan anavyosema katika moja ya hotuba zake.
 
 Zipo sababu kadhaa ambazo huwa zinaelezwa kuwa ni chanzo cha foleni za magari barabarani, zikiwamo ongezeko la umiliki wa magari, wingi wa watu na ukuaji wa idadi ya watu, na kuendelea kukua kwa uchumi.
 
 Vilevile, barabara zilizoko zimepitwa na wakati huku zikiwa na miundombinu duni inayosababisha kuwapo kwa foleni kwa kuwa hazitoshelezi mahitaji ya sasa ya magari yaliyopo.
 
 Ninadhani umefika wakati sasa kuongeza idadi ya njia za kusafiria kwa magari kwa ajili ya kupunguza msongamano au foleni hizo za magari ambazo zimekuwa zikijitokeza katika maeneo mbalimbali ya jiji.
 
 Ikiwezekana, kuwe na barabara nne ambazo wengine wanaziita 'four ways' pamoja na njia za waenda kwa miguu na baiskeli, kwani  kunaweza kusaidia kupunguza foleni zilizoko sasa.
 
 Zimejengwa daraja za juu kwa ajili ya magari kwenye baadhi ya maeneo, kuna mabasi ya mwendo wa haraka, lakini hivyo vyote vimeonekana bado havijawa suluhisho la foleni za magari Dar es Salaam.
 
 Kuna barabara mpya za mabasi yaendayo haraka zinaendelea kujengwa ni vyema, lakini sidhani kama zitaweza kusaidia kupunguza foleni, kwa sababu hakuna miundombinu inayoweza kufanya magari yasikutane.
 
 Ni sawa kama magari yatapishana katika madaraja, lakini yanakutana mbele ya safari na kuweka foleni. Hivyo, ni vyema kuangalia uwezekano wa kuongeza barabara za juu zisizokutanisha magari mbele ya safari.
 
 Wakati huu ambao serikali ina mkakati wa kupunguza kero ya foleni jijini Dar es Salaam, kwa kufanya mazungumzo na kampuni ya kigeni imeonyesha nia kuwekeza mtaji wa Dola za Marekani bilioni moja (Sh.trilioni 2.7) kujenga barabara ili kupunguza foleni hizo, ni vyema kweli foleni zipungue.
 
 Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), David Kafulila, ni kwamba mwekezaji huyo tayari amefanya kazi za awali.
 
 Anataja kazi hiyo ya awali kuwa ni upembuzi yakinifu na uchambuzi wa kiuchumi, na sasa anataka kuingia katika Hati ya Makubaliano na Serikali, ili aweze kufanya upembuzi yakinifu kamili wa mradi huo.
 
 Kafulila anasema kampuni ya COVEC inataka kujenga barabara 10 za mzunguko (ring roads) ikiwa ni pamoja na barabara sita za ndani (inner ring roads) na barabara nne za nje (outer ring roads).
 
 Hivyo, mkakati huo uje matokeo chanya kwenye suala la foleni za magari, kwani zinasababisha baadhi ya watu kuamka mapema kuwa usafiri badala ya kusubiri kupambazuke.
 
 Kwa mfano, wapo baadhi ya watu wanaingia ofisini saa mbili, lakini wanalazimika kuamka saa 11 alfajiri wajiandae ili wawahi usafiri, lakini kama kusingekuwa na foleni wanaweza kuamka hata saa moja kamili.