Yanga yasubiri Aussems aamue

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:44 PM Jul 01 2024
Kocha Mkuu mpya wa Singida Black Stars, Patrick Aussems.
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu mpya wa Singida Black Stars, Patrick Aussems.

KOCHA Mkuu mpya wa Singida Black Stars, Patrick Aussems, anatarajia kuwasili nchini leo kwa kuanza rasmi kazi ya kukinoa kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano, huku akitarajia kuamua hatma ya wachezaji wa timu hiyo wanaotakiwa na Klabu za Simba na Yanga.

Kocha huyo ambaye amewahi kuifundisha Simba 2018 hadi 2019, alipewa kibarua cha kukiongoza kikosi cha timu hiyo kilichobadilisha jina kutoka Ihefu, baada ya kuachana na kocha wake, Mecky Maxime.

Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo, ambayo zamani ikiitwa Ihefu, Muhibu Kanu, amesema, ujio wa kocha huyo mbali na kuanza rasmi kazi ya kufua kikosi hicho, lakini atatoa ripoti kama anaweza kuwaruhusu wachezaji wanaotakiwa na klabu mbalimbali, zikiwamo Simba na Yanga huku ofa zikiwa mezani.

Wachezaji wanaotakiwa kutoka kwenye klabu hiyo ni Elvis Rupia, straika kutoka nchini Kenya, kiungo mshambuliaji Marouf Tchakei raia wa Togo na Emmanuel Lobota, winga raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, na kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma.

"Kuna ofa nyingi mezani, ipo ya Rupia kuna watu wametuma barua ya kuleta ofa, zipo mezani kwangu nimeziona kuna wanaomhitaji Tchakei kuna timu inamtaka Kagoma, hata Lobota, yaani klabu zinataka wachezaji wetu tofauti tofauti, ila tulichokuwa tunasubiri ni kwamba kocha aje, yeye ndiye atatoa ruhusa nani auzwe na nani abakishwe, au wote wabaki, au wauzwe wote wanaotakiwa ili tusajili wengine, kocha ndiye ataamua," alisema Kanu.

Ingawa Kanu hakuweka wazi klabu gani zinawataka wachezaji hao, taarifa za ndani zinasema, Tchakei na Kagoma wanatakiwa na Simba, Lobota amewavutia Yanga na Rupia huenda akatimkia Azam FC.

Kanu amebainisha kuwa kikosi hicho kitaanza rasmi kambi ya maandalizi ya msimu mpya Jumatano ambapo Aussems ataamua sehemu ambayo anataka timu ikajichimbie.