Yanga yaiandalia 'mauaji' KMC FC

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:44 AM Sep 28 2024
news
Picha:Mtandao
Picha:Mtandao

KATIKA kuhakikisha wanazima kasi ya watani zao, mabingwa watetezi, Yanga wameupa kauli mbiu ya 'Jumapili ya Kufosi' mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Hii imekuja saa chache baada ya Simba kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC na kuanzisha vita ya ubingwa wa ligi hiyo wakiwa na lengo la kwenda kuonyesha 'ukubwa wao'.

Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera na ule wa bao 1-0 walioshinda Jumatano iliyopita jijini, Mbeya bado haujawapa furaha wanachama na mashabiki wa Yanga ambao wamezoeshwa ushindi mkubwa na soka safi.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema kesho wanakwenda kukifanya kitu ambacho mashabiki wa Yanga wanapenda, hivyo kuwataka wahudhurie kwa wingi katika mchezo huo.

"Tunakwenda kucheza dhidi ya KMC, inyeshe mvua, liwake jua, wananchi hii ni 'Jumapili ya Kufosi', mpaka kieleweke, tunachokitaka tutakipata," alisema Kamwe.

Yanga ina bahati ya kupata mabao mengi inapocheza dhidi ya KMC, hivyo mashabiki wengi wanaona huenda rekodi inaweza kujirudia.

Agosti 23, mwaka jana, Ligi Kuu msimu uliopita, Yanga iliisasambua KMC mabao 5-0 kwenye uwanja huo huo wa Azam Complex, yakifungwa na Dickson Job, Stephane Aziz Ki, Hafidh Konkoni, Mudathir Yahaya, na Pacome Zouzoua, kabla kupata tena ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili, uliochezwa Februari 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, yakiwekwa wavuni na Mudathir aliyefunga magoli mawili na Pacome akifunga moja.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amebainisha sasa hivi moja kati ya kazi kubwa aliyonayo ni kuboresha viwango vya wachezaji wake kwa sababu wanaonekana kukosa nafasi ya kufunga mabao.

"Tunakosa sana mabao msimu huu, tumelianza kwenye michezo dhidi ya Kagera Sugar, baadaye CBE ugenini, angalau katika mchezo wa marudiano Zanzibar, lakini imejirudia dhidi ya KenGold, nimeanza kulifanyia kazi, nadhani litaondoka muda si mrefu, au litapungua," alisema Gamondi.

Wakati Yanga ikiwa imecheza michezo miwili ikiwa na mabao matatu tu mpaka sasa, watani zao Simba tayari wamefunga magoli tisa katika michezo mitatu waliocheza, huku ikishinda mechi moja mabao 2-0 dhidi ya Azam timu ambayo malengo yake ni kusaka ubingwa, ikichukuliwa pia kati ya timu ngumu nchini.

Kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu jinsi ilivyo na ushindani, si ajabu bingwa anaweza kupatikana hata kwa mabao, hivyo inaonekana Simba na Yanga kutaka kuwekeza kwenye kufunga idadi kubwa ya mabao zaidi msimu huu.