Yanga hasira zote kwa Coastal leo

By Adam Fungamwango ,, Saada Akida , Nipashe
Published at 06:36 AM Apr 27 2024
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi.
Picha; Mtandao
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi.

BAADA ya kulazimishwa suluhu Jumatano iliyopita dhidi ya JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam, Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo wanatarajia kumalizia hasira zao kwa Coastal Union kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, wakisaka pointi tatu zitakazowaweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi, amesema baada ya suluhu hiyo ambayo hawakuitarajia, wana njaa ya ushindi, hivyo wataingia uwanjani kama mbogo aliyejeruhiwa kwa ajili ya kusaka ushindi.

"Tulicheza mechi yetu ya mwisho hali ya hewa ikiwa mbaya, lakini tutaangalia nini kitatokea kesho, najua tutakuwa na mechi ngumu na tutajitahidi kufanya kile kinachotakiwa kufanywa ambacho ni kushinda mechi bila kuangalia nini kimetokea katika mechi iliyopita.

Tuna njaa ya kupata pointi tatu, kwetu ni muhimu, tunajua tunacheza na timu ngumu, inazuia vizuri sana," alisema Gamondi.

Kocha huyo alisema ana uhakika kuwa Coastal Union itakuja na staili ya kupaki basi na kushambulia kwa kustukiza, hivyo amejiandaa na hilo.

"Kuna wakati huwa sipendi sana timu ambazo zinazuia sana kwa sababu mpira ni mchezo wa kuonyeshana ufundi, ustadi wa kushambulia na kutafuta nafasi, lakini zipo timu zina sababu ya kufanya hivyo, hawawezi kupishana, kwa hiyo tunachotakiwa ni kuvunja ngome na kutumia nafasi chache tutakazozipata," alibainisha kocha huyo.

Akizungumzia kuelekea katika mechi ya leo, Kocha Mkuu wa Coastal Union, David Ouma, alisema mechi kwao itakuwa ngumu kwa sababu wanakwenda kucheza na timu iliyokamilika kila idara.

"Tunacheza ugenini na Yanga, tunakwenda kucheza na timu iliyokamilika, kwanza pasi zao, mikimbio yao, wanajua kutumia uwanja vyema, pili ni uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na hilo ndilo tunakwenda kukabiliana nalo.

Kwa hiyo sisi tumejiandaa kwa sababu tumetafuta mbinu ambazo zitatupa faida kwenye hii mechi, kwa sababu tumeshajua tunacheza na timu ya aina gani," alisema kocha huyo.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa, Novemba 8 mwaka jana, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Yanga ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Clement Mzize.

Yanga inayoongoza ligi ikishinda itafikisha pointi 62 ambazo zitaifanya kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuchukua tena ubingwa.

Coastal Union nayo inahitaji ushindi kwa udi na uvumba ili kujishindia katika nafasi ya nne iliyopo.

Timu hiyo ina pointi 33, na kama ikishinda itafikisha 36 na kuikimbia KMC ambayo inainyemelea nafasi hiyo inayotoa uwakilishi wa nchi kwenye michuano ya kimataifa, iwapo bingwa wa Kombe la FA, atapata moja kati ya nafasi tatu za juu.