Waziri Mkuu aita wafanyabiashara Afcon

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:38 AM Jul 25 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

KUFUATIA Tanzania kuwa mwenyeji mwenza wa fainali za Mataifa ya Afrika AFCON mwaka 2027, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya kuwapo kwa fainali hizo hapa nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Majaliwa alisema kuwapo kwa fainali hizo ni fursa kibiashara na kuwataka wafanya biashara wa sekta binafsi kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ili kuzishawishi nchi nyingi kuja kukaa Tanzania kwa ajili ya fainali hizo.

"Fainali hizo pamoja na mambo mengine lakini hii ni fursa ya kibiashara, wenzetu nao tunaoandaa nao pamoja wanafanya mipango ya kuvutia nchi nyingi kwenda kwao, nitoe wito kwa wafanyabiashara wetu kuchangamkia fursa hii," alisema Majaliwa.

Aidha, alisema serikali inajithaidi kuboresha miundombinu ya uwanja ili kuweza kushawishi timu kuja kufanya mazoezi hapa nchini wakati wakijiandaa na fainali hizo.

"Tutaboresha uwanja wa CCM Kirumba, Uwanja wa Majimaji Songea, Uwanja wa Uhuru na Fumba Zanzibar, lengo ni tuvutie mechi nyingi zichezwe Tanzania," alisema.

Alishauri wafanyabiashara kuwekeza kwenye sekta ya hoteli, chakula na usafirishaji kwa kuwa fainali hizo ni fursa kubwa ya kibiashara.

Tanzania itashirikiana kwa pamoja na nchi za Kenya na Uganda kuandaa fainali hizo za mwaka 2027 ambazo kwa mara ya kwanza zitafanyika Afrika Mashariki.