Waziri Junior atua Dodoma Jiji

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:01 AM Jul 26 2024
Waziri Junior.
Picha: Mtandao
Waziri Junior.

KATIKA kile kinachoonekana kujiimarisha kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu, klabu ya Dodoma Jiji imeendelea kufanya usajili wa kishindo ambapo jana mchana ilimtambulisha mshambuliaji wa KMC na timu ya Taifa ya Tanzania, Waziri Junior.

Taarifa iliyotolewa jana na Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, inasema kuwa mchezaji huyo amesaini mkataba wa kuichezea timu hiyo yenye makao yake jijini Dodoma kwa miaka miwili, ambapo mategemeo yao ni kuwa na kikosi bora cha msimu ujao kitakacho himili mikimiki ya msimu.

"Tumepata mali safi, ni Waziri ambaye atakuwa mmoja wa wachezaji wetu wapya watakaounda kikosi chetu kuelekea msimu ujao,"ilisema sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.

Waziri, ambaye amekabidhiwa jezi namba 10 kwenye timu hiyo, ataungana na wachezaji maarufu ambao Dodoma Jiji imefanikiwa kupata saini zao kuelekea msimu ujao ambao ni straika mwenzake, Reliants Lusajo aliyesajiliwa kutoka Mashujaa FC na Ibrahim Ajibu kiungo mshambuliaji wa zamani wa timu za Simba na Yanga, lakini akitokea klabu ya Coastal Union aliyokuwa akiichezea msimu uliopita.

Straika huyo alipachika mabao 12 msimu uliopita na kuongoza kwa ufungaji mabao Ligi Kuu msimu wa 2023/24 kwa upande wa washambuliaji asilia kwani waliokuwa juu yake ni Feisal Salum wa Azam FC aliyefunga mabao 19 na Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyetwaa kiatu cha dhahabu kwa kufunga mabao 21 wote ni viungo.

Mbali na KMC alikotoka, straika huyo amewahi kuzichezea klabu za Toto African, Azam FC, Biashara United, Mbao FC, Yanga na hatimaye timu aliyocheza msimu uliopita inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni, KMC.

Wachezaji wengine wapya ambao wametua Dodoma Jiji FC ni kipa mahiri raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Allain Ngeleka ambaye aliibeba Kagera Sugar msimu uliopita, Dickson Mhilu pia kutoka Kagera Sugar na beki Daudi Milandu kutoka Tabora United.