Wachezaji Simba watoa siri ya Fadlu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:52 AM Jan 13 2025
Kikosi cha Simba.
Picha:Mtandao
Kikosi cha Simba.

HATIMAYE baadhi ya wachezaji wa Simba wametoa siri ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids, kupenda kuwachezesha wote, badala ya kutegemea kundi la wachezaji fulani kikosini.

Wakiwa nchini Angola, wachezaji hao, Awesu Awesu na Kibu Denis, wamesema kocha Fadlu hupanga kikosi chake kutokana na aina ya wapinzani anaokwenda kucheza nao na si kila mchezaji anaweza kucheza kila aina ya mechi.

Wamesema kutokana na tabia yake hiyo, imewafanya wachezaji karibuni wote wawe wanapata nafasi ya kucheza kwa sababu kila mmoja ana kitu chake binafsi kinachompa faida kwenye aina fulani ya mchezo.

"Wachezaji wote tunamuonesha mwalimu ni kitu gani tunacho kwenye mazoezi. Ni sehemu ambayo kocha anaangalia kila aina ya kipaji, uwezo, upambanaji na kitu ambacho anaweza kumpa nafasi kwenye mechi.

"Baada ya hapo kuna mechi zinakuja ambazo anakuhitaji, zipo ambazo anasema kwa aina hii ya mechi hakuhitaji kwa hiyo unakuwa mvumilivu.

"Anatuambia si kila mechi mchezaji anatakiwa acheze. Kila mechi ina aina yake ya uchezaji kulingana na mpinzani unayekwenda kucheza naye," alisema Awesu.

Kwa upande wa Kibu alisema kocha huwa anawaambia kuna michezo anahitaji aina fulani za wachezaji na zingine hawahitaji.

"Anatuambia kuna mechi fulani namhitaji fulani  na mchezo huu simtaki mtu fulani, ambaye hamhitaji anamwambia wewe utanisaidia kwenye mechi nyingine, hivyo unaendelea na mazoezi ili hata siku akija kukupa mchezo, ucheze kwa jinsi ulivyoagizwa na alivyokuona unafaa kucheza mchezo huo," alisema Kibu.

Fadlu, raia wa Afrika Kusini, aliyeichukua Simba kutoka kwa Abdelhak Benchikha raia wa Algeria, ameonekana kuwa mmoja wa makocha kivutio kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa jinsi anavyowatumia wachezaji wake karibuni wote tofauti na watangulizi wake.

Kocha huyo amekuwa akiwachezesha wachezaji ambao hapo awali walionekana kuwa wameshuka viwango kwa makocha wengine.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kocha Fadlu anawapanga wachezaji uwanjani huku kila mmoja akimpa jukumu lake la kufanya na si kwenda kucheza tu.

"Katika mchezo dhidi ya CS Sfaxien, kocha huyo alimpa kazi moja tu Elie Mpanzu, kumtuliza beki wa kulia, Salah Harabi, ambaye alionekana kuwa ndiye chanzo cha mashambulizi yote ya wapinzani wao nchini Tunisia.

"Tulipokuwa ugenini, kocha alimwambia Mpanzu, afanye kazi ya kumkimbiza beki huyo ili asiwe tena na hamu ya kupanda mbele kwa sababu alikuwa ndiye mtu hatari, anapanda kwa kasi, ana spidi na krosi za uhakika, wenyewe ndiyo walikuwa wanamtegemea kwenye mashambulizi, upande uliobaki wa Shomari Kapombe, Kibu Denis akaongezeka na Jean Ahoua ndiyo tukawa tunamtumia sisi kushambulia, tukawazima," alisema Ahmed.